Dar es Salaam. Katikati ya historia ya machafuko katika baadhi ya mataifa ya ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya jumuiya hiyo (MCO), imekuja na mkakati wa Ujenzi wa Taifa na Maendeleo Baada ya Mgogoro (PCRD).
Hatua hiyo, ni sehemu ya juhudi za MCO chini ya uenyekiti wa Tanzania, ikilenga kutumika kama nyenzo madhubuti ya kukabiliana na changamoto za kiusalama kwa mtazamo wa muda mrefu, katika nchi zilizokumbwa na migogoro.
Mkakati huo, unaenda sambamba na mfumo wa kubaini viashiria vya migogoro kabla haijatokea, ambao nao umebuniwa katika mwaka mmoja wa uenyekiti wa Tanzania katika asasi hiyo, unaokoma Agosti mwaka huu na kukabidhiwa kwa Malawi.
Katika ukanda huo, mataifa yanayokabiliwa na migogoro kwa sasa ni Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Kaskazini mwa Msumbiji.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, chini ya uongozi wa Tanzania, SADC imekuwa na jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kuweka msingi wa amani ya kudumu.

Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Mpedi Magosi
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi Julai 24, 2025 na Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, wakati wa kikao cha 27 cha Mawaziri wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema PCRD imekusudiwa kusaidia nchi wanachama kushughulikia vichocheo vya machafuko kama umaskini, kutengwa kwa jamii, utawala dhaifu na ukosefu wa usawa, kabla havijazaa migogoro mikubwa.
“Lengo letu si tu kukomesha migogoro, tunataka kwenda mbali zaidi kufufua maisha ya watu, kujenga upya kwa ushirikishwaji na kusaidia jamii kustawi,” amesema.
Mkakati huo, amesema utasaidia kuhakikisha machafuko ya zamani hayajirudii, hali inayotarajiwa kuvunja machafuko yanayojirudia mara kwa mara na kujenga mustakabali wa amani.
“SADC inaamini kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana bila uponyaji wa kihisia na ushirikishwaji, hasa kwa wale walioumizwa zaidi na migogoro. Hapo ndipo dhana ya haki mpito na maridhiano yanayoongozwa na jamii inapochukua nafasi,” amesema.
Magosi amesisitiza uwekezaji katika programu za urejeshwaji na uunganishwaji wa waathirika wa migogoro utakuwa muhimu.
“Haki siyo tu kuadhibu wahalifu, bali ni kuisaidia jamii kupona na kuwajengea watu fursa mpya za maisha,” ameeleza.

Kwa mwaka huu, Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma mikakati ya muda mrefu ya usalama chini ya uongozi wa Waziri Thabit Kombo ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa wa kamati hiyo ya mawaziri.
Tanzania imetekeleza asilimia 70 ya maazimio ya Baraza la Mawaziri wa SADC, kitendo kinachodhihirisha hatua ya mafanikio katika kujenga na kudumisha amani na usalama katika ukanda huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Tanzania pia ni miongoni mwa nchi mbili zinazotazamwa kuwa kielezo cha juhudi za kupambana na rushwa katika ukanda huo.
Amesema jitihada nyingine muhimu ni kuendelea kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kukabiliana na Ugaidi (RCTC) kilichopo Dar es Salaam, taasisi inayotajwa kuwa nguzo ya usalama wa ukanda kupitia uratibu, kubadilishana taarifa za kiintelijensia na mafunzo ya uwezo wa kitaifa na kikanda.
Hatua nyingine ya kupongezwa, amesema ni kuzinduliwa kwa Mtandao wa Wanawake Wapatanishi mapema mwaka huu.
“Hii ni hatua muhimu sana. Wanawake wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa amani. Sauti zao ni muhimu hasa kwa kuzingatia mahitaji ya watoto na makundi mengine yaliyo hatarini,” amesema.
Wakati huohuo, amesema SADC pia inaongeza juhudi za kukabiliana na vitisho vya usalama vinavyovuka mipaka, kama ujangili, biashara ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu, uhalifu wa mtandaoni na biashara ya silaha na magari.

Mnamo Juni 2025, Wakuu wa Polisi wa nchi wanachama walikubaliana kuongeza ushirikiano wa kiintelijensia na kufanya operesheni za pamoja ili kukabiliana na uhalifu huo.
Rushwa pia imetajwa kama kikwazo kikubwa katika juhudi za kudumisha amani na maendeleo.
Waziri Kombo amesema nchi wanachama sasa zimeanza kutekeleza mkakati wa kupambana na rushwa wa SADC, huku Tanzania na Mauritius zikiendelea na majaribio ya kielezo kipya cha tathmini ya juhudi dhidi ya rushwa.
Katika kukabiliana na ugaidi, Waziri Kombo amesisitiza umuhimu wa kukiimarisha kituo cha RCTC kwa kukipatia vifaa na fedha stahiki ili kutimiza majukumu yake kikamilifu.
“Tanzania inapojiandaa kukabidhi kijiti cha uenyekiti kwa Malawi, mchango wake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita utabaki kuwa wa kihistoria, si tu kwa kushughulikia migogoro ya sasa, bali pia kwa kuweka msingi imara wa amani ya baadaye,” amesema.
Amesema tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipochukua uenyekiti wa asasi hiyo Agosti 2024, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kusimamia na kushughulikia changamoto mbalimbali za amani na usalama.
“Imani yetu inabaki palepale kwamba, matatizo ya Afrika ni lazima yashughulikiwe na Waafrika wenyewe. Na kupitia mikakati kama PCRD, tupo karibu zaidi kufanikisha ndoto hiyo,” amesema