Serikali yapiga marufuku jezi feki CHAN 2024

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imewataka Watanzania kuhakikisha wanavaa jezi sahihi za timu ya taifa ‘Taif Stars’ katika kipindi chote cha Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika kuanzia Agosti 2 hadi Agosti 30 mwaka huu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ameyasema hayo katika uzinduzi wa mfumo maalum wa Duka Mtandao wa kampuni ya Vodacom ambao unawezesha uuzaji wa jezi za Taifa Stars kwa njia ya mtandao.

“Tunatakiwa kununua jezi ambazo sio feki kwa sababu mapato yake pamoja na mambo mengine yanalipa kodi na yanakwenda kusaidia timu ya taifa. Ni matumaini yangu kwamba kama tutafanya vizuri kama tunavyotarajia kwenye CHAN hata ile nafasi ya kufungua AFCON 2027 ambayo tutaandaa nchi tatu pamoja na Kenya na Uganda tutaipata,” alisema Mwana FA.

Mwana FA pia ameomba taasisi, mashirika na kampuni mbalimbali kuanzisha utaratibu kwa wafanyakazi wake kuvaa jezi za Taifa Stars kila siku ya Ijumaa ili kuhamasisha uzalendo kwa timu hiyo.

Mshauri wa Sandaland, Imani Kajula amesema kuwa jezi ni utambulisho mzuri wa uzalendo na sapoti kwa timu ya Taifa.

“Tuna wajibu wa kuhakikisha tunaweka hamasa kwa Watanzania kuisapoti timu yao,” alisema Kajula.