Sh250 milioni kuwafadhili wanafunzi wenye vipaji

Dar es Salaam. Benki ya Diamond Trust Tanzania Plc (DTB) imetoa msaada wa Sh250 milioni kwa Huduma ya Elimu ya Aga Khan Tanzania (AKES) ili kusaidia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaosomea Mpango wa Diploma ya Kimataifa ya International Baccalaureate (IB).

Mpango huo unawalenga wanafunzi wa Kitanzania wenye vipaji, hususan kutoka katika mazingira yasiyo na uwezo wa kifedha, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Makabidhiano hayo yametangazwa jana, Jumatano, Julai 23, 2025, na Mkurugenzi Mtendaji wa DTB Tanzania, Ravneet Chowdhury.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa AKES Tanzania, Dk Shelina Walli, pamoja na Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ally Mussa.

Chowdhury amesema mpango huo wa ufadhili unatokana na makubaliano ya ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa mapema mwaka huu kati ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) na taasisi ya International Baccalaureate.

“Ushirikiano huo unalenga kuongeza upatikanaji wa elimu bora katika nchi za Kusini mwa Dunia (Global South) na kukuza ubunifu wa mitaala, mafunzo yenye misingi ya maadili na umuhimu wa muktadha wa ndani,” amesema.

Ameongeza kuwa katika AKES Tanzania, mitaala ya IB imeunganishwa na kujifunza kwa matendo kupitia miradi ya kijamii kama vile urejeleaji wa taka, utengenezaji wa mboji, na ziara katika maeneo ya kiutamaduni, ili kukuza uelewa wa mazingira na uwajibikaji wa kiraia sambamba na ubora wa kitaaluma.

“Kuwawezesha vijana kupitia elimu ni msingi wa kujenga viongozi wa baadaye wa Tanzania,” amesema Chowdhury. “Kwa kuondoa vikwazo vya kifedha, tunafungua uwezo wao na kuunda njia za mafanikio ya kimataifa.”

“Pamoja, tunashirikiana katika kufanikisha malengo yetu na kuendeleza usawa, ubora na ustawi katika soko la Tanzania ambako tunatekeleza biashara zetu,” amesema.

Amesema mafunzo kwa vitendo pia hufanyika, ambapo wanafunzi hutumia maarifa yao katika miradi inayochangia jamii yao. Kwa mfano, wanafunzi huongoza juhudi za kuchakata chupa za plastiki, kutengeneza mbolea ya mimea, kutembelea maeneo ya utamaduni kama Maasai Boma na kushiriki katika maonyesho mbalimbali ya sanaa.

“Jitihada hizi zinakuza uwajibikaji wa mazingira, kuthamini tamaduni na ushiriki wa kijamii. Uwezeshaji wa vijana kupitia elimu ni jambo muhimu katika kujenga hazina thabiti ya vipaji vya viongozi wa baadaye wenye maono ya kuipeleka Tanzania katika viwango vya juu zaidi kiteknolojia na kiuchumi, kama ilivyoelezwa hivi karibuni katika Dira ya Maendeleo 2050,” amesema.

Akifafanua, amesema kuwapunguzia wanafunzi vikwazo vya kifedha na kutoa nafasi kwa wanafunzi wenye vipaji na akili kutoka familia zenye uhitaji, watakuwa wamefungua milango na kuunda fursa endelevu kwa vijana wa Kitanzania kustawi na kuwa wataalamu wenye uwezo kamili wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.

“Pamoja, tunashirikiana katika kufanikisha malengo yetu na kuendeleza usawa, ubora na ustawi katika soko la Tanzania ambako tunatekeleza biashara zetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AKES Tanzania, Dk Walli, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo.

“Safari yetu ilianza mwaka 1905 kwa kuanzishwa kwa shule ya kwanza ya Aga Khan huko Zanzibar. Urithi huu unaendelea tunapochanganya nguvu za NECTA za Tanzania na mipango ya kimataifa kama IB siyo kwa ajili ya kuchukua nafasi, bali kuimarisha, kuinua na kuendana na mageuzi ya kitaifa.”

Amesema msaada kutoka DTB tayari unaendelea kubadilisha maisha: “Mmoja wa wanafunzi wetu wa IB, ambaye awali alisoma katika mfumo wa NECTA, ameonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kutambuliwa na jamii ya kimataifa ya IB kupitia mradi wake wa kulenga Dar es Salaam kama jiji la mfano.”

Amesema DTB na AKES Tanzania watafuatilia kwa karibu athari za ufadhili huo ili kuhakikisha unawafikia wanafunzi wanaostahili zaidi, na kuwa mfano kwa sekta binafsi kushiriki katika elimu na maendeleo endelevu.