Sh500 milioni  kuwawezesha wakulima wa karafuu Zanzibar 

Unguja. Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea) umesema hautoi mikopo kwa wananchi pekee badala yake unajipanga kutoa elimu ya kifedha ili fedha ili itumike kwa malengo kusudiwa.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Julai 24, 2025 kisiwani Unguja na Mkurugenzi wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed wakati wa utiaji saini hati ya makubaliano baina ya wakala huo na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC.

Amesema elimu hiyo ya fedha kwa wananchi itawasaidia kukopa  na kurejesha ili na wengine wanufaikie na mikopo hiyo. 

“Hizo ni fedha za mikopo hivyo wakulima wa karafuu mnapaswa kuzitumia kama tulivyokubaliana na sio kinyume chake na kuhakikisha zinarudi,” amesema Juma. 

Juma amesema kupitia ushirikiano huo, ZEEA imetenga Sh500 milioni kwa wajasiriamali wa kilimo cha karafuu na unalenga kuleta mageuzi kwa wakulima hao ili kuongeza uzalishaji na kujiinua kiuchumi.

Amefafanua kuwa lengo la kusaini mkataba huo ni kukuza sekta ya kilimo hasa cha karafuu kwani Taasisi hiyo imekuwa ni suluhisho la kutatua changamoto za wajasiriamali.

Vilevile, ametoa wito kwa watendaji wa taasisi hiyo   kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wakulima ili mikopo hiyo itolewe katika muda uliotakiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC, Soud Said Ali amesema hiyo ni hatua muhimu kwa shirika hilo kwa kupata mshirika atakayesimamia utoaji wa mikopo kwa wakulima wa karafuu. 

Amesema, awali shirika hilo lilikuwa likitoa mikopo lakini kuna baadhi ya mapungufu yalijitokeza ambapo waliamua kusitisha na kutafuta mtaalamu wa utoaji mikopo.
Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa mikopo hiyo haitakuwa na  upendeleo wowote, itatolewa kwa kila mmoja atakayekidhi vigezo vinavyohitajika.