Siasa za uchaguzi zatawala ibada ya kumuaga Mama Makete

Dar es Salaam. Ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Wilaya ya Kinondoni, Anna Hangaya maarufu Mama Makete imetawaliwa na vimbwanga, kicheko na siasa za michakato ya uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho.

Ni jambo ambalo kwa hali ya kawaida usingedhania, pengine kungetawala kilio na simanzi, lakini huo ndio uhalisia uliojiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Tegeta Usharika wa Wazo Hill, ilikofanyika ibada ya hiyo ya mwisho ya kuaga mwili huo kabla ya kwenda kuzikwa nyumbani kwake Nyakasangwe Mtaa wa Havanna.

Mama Makete aliyekuwa mfanyabiashara aliyejipatia umaarufu zaidi wakati wa uhai wake kutokana na kauli za mahaba yake kwa CCM kwamba anaipenda kuliko anavyowapenda watoto wake, alifariki duni Julai 21, 2025 wakati akipatiwa matibabu ya maradhi ya saratani ya mapafu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na makada, viongozi wa CCM na wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, hali ilianza kubadilika baada ya Katibu wa Siasa na Uenezi CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga kupewa kipaza sauti kutambulisha viongozi.

Bananga alianza kusema: “Hapa inabidi nijitahidi nitaje kila jina la kiongozi na watiania na watia huruma, ili kuepuka nongwa vinginevyo nitatumbukia kwenye lawama nzito maana najua na nawajua nyote…” amesema Bangana

Wakati anaanza kutambulisha huku umma unacheka kuna wakati aliwasahau baadhi ya makada watiania na Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba.

“Naomba mnisamehe jamani sijawasahau ila wakati mnakuja hatukuonana, msinipandikizie maneno, kipindi hiki cha watiania na watia huruma kina nongwa zaidi, hasa nyie wajumbe,” amesema.

Chalamila aliunga mkono kilichosemwa na Bananga kwa hoja aliyoijenga kuwa na yeye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa na watiania wakishajadiliwa ngazi ya chini hatua inayofuata huwa anashiriki.

“Hiki alichosema ndugu yangu Bananga ni sawa kabisa kuhusiana na wale watiania hata Mama Makete alishiriki kuwajadili na mwisho kutoa mapendekezo yake.

Juzi nilisoma mahali Mungu aliumba dunia siku sita lakini siku ya saba alipopumzika shetani aliiba udongo na kwenda kuumba wajumbe,” amesema Chalamila huku waombolezaji wakiangua kicheko.

Chalamila amesema wale ambao alishiriki kuwajadili ndiyo wale kwa mujibu wa kale ‘kataarifa alikosema Bananga.’

“Nimeamua kuyasema haya, kama ambayo wanasema kiimani misiba yote ni misiba lakini msiba wa mwanamke unauma zaidi nitoe neno la faraja kwa familia,” amesema.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Richard Kasesela amesema katika kipindi cha mchakato wa ndani unaendelea ndani ya chama hicho hakuna ambaye hajatenda dhambi, huku akiwataka wagombea wamrudie Mungu.

“Nina maana yangu kipindi hiki watu wamekiuka mniruhusu niisome: “Nawe usipokee rushwa, kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hawa waonao na kuyapotosha maneno ya wenye haki na nina uhakika hata ukisema ushahidi naweza nisilete lakini kipindi hiki watu wamevuna sana.”

“Kuna waliovuna kanga, mifukoni sana, lakini naomba zisiwapofushe macho katika kuchagua viongozi bora na wanaoweza kuwasaidia,” amesema Kasesela

Alimtaka mchungaji kiongozi wa Usharika huo kuandaa ibada  baada ya mchakato wa kupata viongozi ndani ya chama hicho utakapokamilika ili kutoa fursa kwa waliotenda dhambi wakatubu.

Katika hatua nyingi, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya UWT-Tanzania, Zainabu Shomary amesema kifo hicho kimewagusa kwani alikuwa mshauri na aliyekuwa na upendo mkubwa.

“Wakati wote mama huyu alisimama kwa imani dhabiti, hata mwenyewe katika uchaguzi wetu alisimamia kuhakikisha tunashinda kwa kishindo, ni muhimu kuendelea kuyaenzi maisha yake kwa vitendo,” amesema.

Zainabu amewasihi Watanzania kuyaishi maisha yake kwa vitendo, upendo kwani alikuwa habagui alikuwa anaamini binadamu wote ni sawa.

Awali, Mwenyekiti wa CCM, Kinondoni, Shaweji Mkumbura amemzungumzia marehemu alikuwa ni zaidi ya kiongozi na katika harakati zote za kisiasa zilizofanyika hususani mwaka jana alipoanza kuumwa akuacha kutushauri.

“Kinondoni tumefiwa, na namna pekee ya kumuenzi basi ni kukipenda chama kwa mapenzi ya dhati lakini ni mtu ambaye alikuwa na msimamo wake katika jambo alilokuwa analiamini,” amesema Shaweji.

Katika mahubiri, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Wazo Hill, Herman Kiporoza amesema marehemu ulitumika kila mahali, ikiwemo kanisani na kwenye chama chake, hivyo alijiandaa kwenda mbinguni.

“Ni msiba unaoumiza na unaogusa wengi kwa kuwa ulitumika maeneo mengi, kifo hakijawahi kuzoelekea, ni muhimu tusisahau tukiwa hai kutenda mema na katika jambo, lililopotea kwa sasa katika jamii zetu hakuna mashirikiano ya wengine hawataki kugusa maisha ya wengine,” amesema.

Amesema marehemu amelala watu wanang’ang’aniana wamuage kwa namna gani, ni muhimu kujenga ushirikiano kwani duniani kila mmoja alikuja bila kitu na ataondoka bila chochote.

“Sadaka ya matendo mema ndiyo huwa inampendeza Mungu, kila mmoja ajiulize matendo yake yakoje? na ikiwa wewe ungelala nani angekuaga ni muhimu kuweka faili lako vizuri ili usije kutesa watu baadaye,” amesema.

“Amemaliza mwendo akiwa ameacha alama, hata mwenyewe Ijumaa nilikuwa naye Ocean Road nilienda kumuombea lakini matakwa ya Mungu anayajua mwenyewe.”

Mioyo yetu inaweza kuumia lakini lazima tujue duniani tu wapitaji, hakuna mji unaodumu hivyo ni wakati wa kujua kumsujudia Mungu nyakati zote.

Wasifu, marehemu Anna amefariki dunia akiwa na miaka 71, ameacha watoto watatu kati ya hao wawili wa kiume.