MIAKA mitatu tu iliyopita jina la Victorien Adebayor lilikuwa maarufu katika ardhi ya Tanzania ingawa mchezaji huyo wa Niger alikuwa hachezi katika klabu ya hapa nyumbani.
Kiwango bora alichokionyesha katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambalo timu yake ya Gendarmerie kiliikosha Simba ambayo ilitajwa kuanza harakati za kumuwania ikiamini ataimarisha kikosi chake.
Kiukweli kwa mtu yeyote mwenye akili timamu asingeweza kuishangaa Simba kumhitaji Adebayor kipindi kile maana pamoja na kucheza nafasi ya winga, alikuwa tishio katika kufunga mabao kwani alipachika mabao sita katika hatua ya makundi ingawa timu yake ilishika mkia.
Hata hivyo juhudi za Simba kumnasa ziligonga mwamba licha ya ushawishi uliofanywa hadi na mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wakimuimba mitandaoni na pindi alipokuja kucheza hapa.
Mwaka jana, ndoto za Adebayor kucheza Tanzania zikatimia ingawa hakusajiliwa na Simba bali alijiunga na Singida Black Stars na kijiwe kilitegemea angetumia fursa hiyo kukonga nyoyo za Watanzania na kuthibitisha kuwa jina lake hapa hakulipata kwa bahati mbaya.
Labda kama alikuwa na hamu ya kuchezea Simba, hiyo ilikuwa ni nafasi nzuri kwake kutengeneza mazingira kwa kufanya vizuri na kuwashawishi vigogo wa miamba hiyo ya soka kuingia kazini kuisaka saini yake.
Lakini mambo yamekuwa tofauti na licha ya kuingia akiwa na jina kubwa, ameshindwa kuonyesha kiwango bora na leo hii hapa kijiweni tumesikia Singida Black Stars iko katika mpango wa kumfungulia mlango wa kutokea ili apishe nyota mwingine wa kigeni.
Inaonekana kama Adebayor aliichukulia poa Singida Black Stars na soka la Tanzania kijumla akiamini angeweza kulinda ustaa wake bila kuvuja jasho katika viwanja vya mazoezi na kuonyesha kiwango bora katika mechi.
Mwishowe, amekumbushwa kuwa soka la Tanzania kwa sasa siyo lelemama na ukija kizembe zembe utarudi kwenu haraka iwezekanavyo tofauti na unavyotegemea