Stamico yapewa leseni ya utafiti na uchimbaji madini adimu

Morogoro: Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuharakisha mchakato wa uendelezaji wa leseni waliyokabidhiwa ya utafiti na uchimbaji madini adimu na muhimu katika kilima cha Wigu kilichopo Kijiji cha Sesenga Tarafa ya Bwakila, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Mavunde ametoa agizo hilo wakati wa hafla  ya makabidhiano ya leseni ya utafiti na uchimbaji madini adimu na muhimu kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 15.4 (sawa na ekari 3,557) lilitengwa tangu mwaka 2015 kwa ajili ya utafiti wa madini hayo.

Amesema uamuzi huo umekuja baada ya Serikali wa kuirejesha leseni hiyo kutoka kwa kampuni ya Wigu Hill Mining Company Limited baada ya kumalizika kwa shauri la madai kwenye Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji ICSID).

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara kwenye hafla ya makabidhiano ya leseni hiyo, Waziri Mavunde amesema kuwa madini hayo ni  ya kimkakati na kwa sasa yanahitajika kwa kiwango kikubwa duniani kutokana na umuhimu wake katika sekta ya teknolojia ya kisasa.

“Madini haya yanatumika katika vifaa vya kivita, kutengeneza simu janja, kompyuta, betri za magari ya umeme, vifaa vya matibabu na mashine mbalimbali. Hii ni fursa adhimu kwa kijiji cha Sesenga, na Taifa kwa ujumla kunufaika na rasirimali hii muhimu,” amesema Mavunde.

Waziri huyo  amebainisha kuwa mradi huo utafungua fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa maeneo ya jirani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaozunguka mgodi kuuza bidhaa zao mgodini, na kupitia uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Vilevile, ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro itaongeza mapato yake kupitia tozo za huduma ambazo hutozwa kwenye shughuli za madini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse amesema shirika hilo liko tayari kuanza kazi kwa wakati na kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi, kwa muda uliopangwa na kwa kuzingatia manufaa mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Tunatambua wajibu wetu mkubwa kwa Taifa, Stamico iko tayari kusimamia mradi huu kwa weledi wa hali ya juu ili kuleta tija na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa,” amesema Dk Mwasse.