Taifa Stars yawekewa Sh1 bilioni Chan 2024

KATIKA kuongeza hamasa ya kufanya vizuri kwenye Fainali za Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024, wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars mezani wamewekewa kitita cha Sh1 bilioni endapo watatwaa ubingwa.

Michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Agosti 2 hadi 30 mwaka huu, Tanzania ni nchi mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Taifa Stars iliyopangwa Kundi B, itafungua dimba la michuano hiyo kwa kucheza dhidi ya Burkina Faso kwenye Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Agosti 2.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi, amesema: “Katika kuchagiza hamasa kwa timu yetu ya Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya donge nono la fedha za Kitanzania shilingi bilioni moja kwa vijana wetu wa Taifa Stars iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano haya ya CHAN 2024.”

Aidha, Kabudi amezungumzia maandalizi ya Chan 2024 yalipofikia kwa upande wa Tanzania ambapo amesema kuna hatua nane zimeshafikiwa.

Akizitaja hatua hizo, Kabudi amesema: “Moja ni kukamilisha malipo ya gharama za ada ya ushiriki na fedha za maandalizi. Pili, kufanikisha maandalizi ya viwanja vya mashindano na viwanja vya mazoezi Dar es Salaam na Zanzibar kwa asilimia 100.”

Hatua ya tatu ni kuandaa kamati za kitafaifa za maandalizi ya mashindano hayo na nne ni kuratibu maandalizi ya Taifa Stars.

“Tano ni kuwajengea uwezo wataalamu wetu watakaohusika na uratibu na usimamizi wa mashindano hayo. Sita ni kuandaa mkakati wa hamasa na kutangaza mashindano hayo.

“Jambo la saba ni kukamilisha maandalizi ya huduma muhimu za kijamii, kama vile huduma za malazi, usafiri, hospitali kwa timu zote shiriki, viongozi wa CAF na wageni watakaokuja kushuhudia mashindano hayo na mwisho ni kukamilisha maandalizi muhimu kuelekea mechi ya ufunguzi.”

Katika hatua nyingine, Kabudi amewataka Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara na uchumi kutokana na uwepo wa michuano ya Chan 2024.

“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara na kiuchumi zinazoambatana na mashindano haya ikiwemo malazi, utalii, vyakula na usafirishaji.

“Aidha niwaombe wapezi wa washabiki wa mpira wa miguu wa jijini Dr es Salaam na maeneo yote nchini kujitokeza kwa wingi wetu ili kuwapa hamasa vijana wetu kufanya vizuri ili Kombe libaki Tanzania kama kauli mbiu yetu ambayo tuliizindua pale Mbagala Zakhiem inavyosema (LINAKUJA NYUMBANI),” amesema Kabudi.

Taifa Stars ipo Kundi B ambapo mechi zake zitachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa huku viingilio vikiwa ni kuanzia Sh2,000 (jukwaa la mzunguko), Sh5,000 (VIP B) na Sh10,000 (VIP A). Timu zingine zilizopo kwenye kundi hilo ni Burkina Faso, Madagascar, Mauritania na Jamhuri ya Afrika ya Kati.