Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema Tanzania ina kila sababu ya kupiga hatua kwenye biashara nje ya nchi kupitia soko huru barani Afrika.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 24, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), hafla iliyowakutanisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali.
AfCFTA ni mpango wa Umoja wa Afrka (AU), uliosainiwa na nchi 54 kati ya nchi 55 wanachama wa AU, ukilenga kuunda soko moja lenye lengo la kuwaunganisha watu wote kwa kuondoa vizingizi vya kibiashara ikiwemo vya kiushuru wa forodha.
Hivyo, amewaomba wafanyabiashara, kampuni changa bunifu na wajasiriamali nchini kuchangamkia fursa hiyo kuuza bidhaa zao nje kwa lengo la kuongeza uchumi kupitia fedha za kigeni.
Amesema miundombinu ya ufanyabiashara ikiwemo reli, bandari, viwanja vya ndege, uthibitishaji wa ubora wa bidhaa, mifumo ya malipo ambayo ni sehemu muhimu za kusafirisha bidhaa nchi mbalimbali ipo tayari.
“Kuna kampuni zaidi ya 43 za Tanzania zinashiriki huku zikifanya biashara katika nchi 18. Kuna watu bilioni 1.4 barani Afrika, hivyo ni fursa kwa Watanzania ikiwa ni fursa ya kimaendeleo,” amebainisha.
Kupitia mpango huo, Tanzania inauza bidhaa katika nchi za Misri, Nigeria, Algeria bidhaa kama kahawa, mchele.

Akifafanua zaidi, Waziri Jafo amesema sasa ni wakati wa Watanzania kushirikia katika soko jipya kuongeza thamani ya bidhaa zao na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema sekta ya uchukuzi ambayo ni mishipa ya uchumi inatambua unyeti wa sekta ya biashara, hivyo inaendelea kutengeneza mazingira bora ya kuunganisha bara ikiwemo ujenzi wa meli, viwanja vya ndege na reli.
“Kuna nchi nane zinategemea Tanzania, hivyo miradi kama SGR, bandari na ujenzi wa meli mpya zote ikiwa ni juhudi za kuunganisha nchi kama Burundi, Congo, DRC, Kenya, Uganda, Sudan ili kuwawezesha wafanyabiashara,” amesema Kihenzile.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema vijana ndio wenye dhamana ya kutekeleza mkakati huo kwa kuwa ndio nguvukazi ya taifa.
Awali, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango kutoka Shirika la Viwango (TBS), David Ndibalema amesema ili bidhaa kuvuka mipaka katika soko hilo lazima ziwe zimethibitishwa ubora wake na Tanzania ni mwanachama wa kuandaa ubora wa viwango ili kukidhi viwango vilivyowekwa.
Amesema kinachofanyika hivi sasa ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo kukidhi viwango vya kuvuka mipaka ya nchi.
Naibu mwakilishi mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), John Rutere amesema shirika litaendelea kuunga mkono utekelezaji wa biashara hiyo ya Afrika.
“UNDP kama mdau wa maendeleo yuko tayari bega kwa bega kushirikiana katika mkakati huu kwa ajili ya maendeleo,” amesema Rutere.
Akiwakilisha Balozi wa Japan, Mkuu wa Ushirikiano ubalozi wa Japan, Hashimoto amesema Japan itaendelea kufadhili mkakati huo kwa kuwa inaamini ni sehemu ya uwekezaji, kufanya biashara na maendeleo ya kiuchumi.