TBA yaja na mkakati utekelezaji wa Dira 2050

Dar es Salaam. Katika hatua inayochangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) na Chama cha Watoa Huduma za Fedha kwa Njia ya Kidijitali(Tafina) wamesaini makubaliano yenye lengo la kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuboresha usalama wa mifumo ya kifedha nchini.

Dira ya 2050 iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 17, 2025 inalenga kuijenga Tanzania ya baadaye inayotegemea ubunifu wa kidijitali kwa ajili ya tija, ustawi wa wananchi, na ujumuishaji wa kifedha kwa wote.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Tuse Joune, akizungumza na waandishi wa habari jana Alhamisi, Julai 23, 2025 amesema ushirikiano huo unakusudia kupanua huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali, kulinda watumiaji dhidi ya hatari za kimtandao, na kuchochea ubunifu unaolenga kuleta maendeleo jumuishi.

“Makubaliano haya si ushirikiano wa kawaida bali ni mpango wa kujenga mustakabali mpya ambapo teknolojia na usalama vinakwenda sambamba kwa manufaa ya kila Mtanzania,” amesema Joune.

Ushirikiano huo pia unalenga kusaidia utekelezaji wa mikakati ya kitaifa kama Mfumo wa Tatu wa Kitaifa wa Ujumuishaji wa Kifedha (2023–2028) na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDMP) 2020/21 – 2029/30, ambayo yote inasisitiza umuhimu wa ubunifu na ushirikiano katika kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha.

Ingawa ripoti ya FinScope 2022 inaonesha ujumuishaji wa kifedha umefikia asilimia 89, sekta rasmi ya mabenki bado inahusisha asilimia 22 pekee ya watumiaji.

Kupitia ushirikiano huu, TBA na Tafina wanalenga kupunguza pengo hilo kwa kubuni suluhisho za kidijitali zitakazowafikia makundi yaliyo pembezoni, wakiwemo wakulima wadogo, jamii za vijijini, watu wenye ulemavu, wanawake, na vijana.

Meneja wa Ushirikiano wa Tafina, Julieth Kiluwa amesema makubaliano hayo ya kimkakati yanaashiria dhamira ya pamoja ya kutumia teknolojia kama nyenzo ya kukuza uchumi jumuishi na maendeleo endelevu.

“Makubaliano hayo yatafungua milango ya ushirikiano katika utafiti wa pamoja, ubunifu wa sera, na utengenezaji wa bidhaa zinazolenga mahitaji ya jamii lengo ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika mabadiliko ya kidijitali ya taifa,” amesema Kiluwa.

Amesema ushirikiano huo unajumuisha kuwekwa kwa mikakati ya kuimarisha ufanisi wa mifumo ya kifedha kuimarisha utiifu wa kanuni za udhibiti, na kuharakisha matumizi ya teknolojia za kifedha zilizo salama na za kisasa.

Kwa mujibu wa viongozi wa mashirika hayo, ushirikiano huu unaweka msingi wa mabadiliko ya muda mrefu katika sekta ya fedha, huku ukiunga mkono jitihada za kujenga mfumo wa kifedha wa kisasa unaoendana na maono ya Tanzania ya 2050.