Tisa wanaswa na Takukuru Mara, tuhuma za rushwa uchaguzi CCM

Musoma. Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara imewakamata na kuwahoji makada tisa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiwepo wagombea udiwani viti maalumu kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Makada hao wanatuhumiwa kuhusika na kutoa rushwa kwa wajumbe wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho uliofanyika Julai 20, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Alhamisi Julai 24, 2025, Mkuu wa Takukuru mkoani humo, Mohamed Shariff amesema makada hao wanadaiwa kutoa rushwa kinyume cha sheria na taratibu.

Amesema uchunguzi dhidi ya watuhumiwa hao unaendelea na upo katika hatua mbalimbali.

Amefafanua kuwa wagombea wawili wa nafasi ya udiwani viti maalumu kutoka katika Manispaa ya Musoma wanadaiwa kutoa rushwa ya fedha na kanga kwa wajumbe wa mkutano mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kama kishawishi cha kupigiwa kura.

“Tulikamata pia, makada wengine saba kule Musoma vijijini wawili wanawake na watano wanaume walikuwa na gari aina ya Noah wakigawa fedha kwa wajumbe, hawa ni wapambe wa baadhi ya wagombea,” amesema.

Hata hivyo, Shariff amekataa kutaja majina ya watuhumiwa hao kwa madai kuwa uchunguzi bado unaendelea, ingawa taarifa zilizopo zinaeleza kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao wapo walioshinda kwenye kura za maoni zilizofanyika Julai 20, 2025.

Amesema uchunguzi huo umechukua muda kukamilika kutokana na sababu kadhaa ikiwemo hitaji la kuwapata viongozi wa watuhumiwa kichama ili kupata ufafanuzi wa maadili ya kichama kulingana na kanuni zao za uchaguzi.

“Hapa maana yake ni kuwa tunalazimika kuwahoji viongozi wa chama lakini kwa sasa kuwapata ni kazi ngumu kutokana na mchakato unaoendelea, jambo jingine ni hitaji la kupata nyaraka au taarifa za ushahidi wa kitaalamu kutoka mamlaka husika kama vile benki na kampuni za simu,” amesema.

Amesema uchunguzi ukikamilika mbali na kuchukua hatua zingine, pia, watatoa mapendekezo yao kwa chama kuhusu watuhumiwa hao ili kiamue kama wanafaa kuwa viongozi au la.

Ametoa wito kwa wagombea kuacha kufanya vitendo hivyo kwa maelezo kuwa kuepukana na rushwa ni kujijengea heshima na sifa ya uadilifu kwa wananchi wanaokusudia kuwaongoza.

Baadhi ya wakazi wa Musoma akiwamo Editha Ntabuzi wameipongeza Takukuru kwa hatua hiyo huku wakitaka watuhumiwa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi.