Iringa. Mradi wa kimkakati wa Tanzania- Zambia (Taza) unaolenga kuunganisha nchi hizo mbili kupitia njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa hadi Sumbawanga umefikia asilimia 60 upande wa njia ya kusafirisha umeme
Aidha, kwa vituo vya kupoza vimefikia asilimia 31 ya utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya Sh2 trilioni. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange amewataka wakandarasi wanaoutekeleza kuzingatia masharti ya kimkataba.
Njia hiyo itakuwa ikisafirisha umeme kupitia Taza na kuunganisha Tanzania na Zambia, hatua inayotarajiwa kuongeza usambazaji wa nishati na kuongeza mapato ya Serikali kupitia njia kuu za umeme nje ya nchi.

Viongozi mbalimbali wa Tanesco, wakandarasi wakiongizwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Lazaro Twange (watatu kutoka kulia) wakikagua mradi wa kimkakati wa TAZA unaolenga kuunganisha Tanzania na Zambia.
Akizungumza jana Jumatano, Julai 23, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Iringa, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange amesema mradi huo ni wa kimkakati kwa maendeleo ya taifa na uhusiano wa kikanda.
“Nimekuja kukagua maendeleo ya Mradi wa Taza unaoanzia hapa Iringa hadi Sumbawanga. Huu ni mradi mkubwa na muhimu kwa taifa letu kwa sababu unakwenda kuimarisha usambazaji wa umeme ndani na nje ya nchi,” amesema Twange.
Katika ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Tanzania – Zambia (Taza) katika mikoa ya Iringa na Njombe, hasa maeneo ya ujenzi wa njia ya umeme na vituo vya kupoza umeme vya Tagamenda na Kisada, Twange amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu unazingatia muda wa kimkataba ili kukamilika kwa wakati.

Aidha Twange amesisitiza mradi huo ni wa kimkakati kwani utafungua fursa ya biashara ya umeme kati ya Tanzania na Zambia, hivyo ni lazima ukamilike kwa ufanisi na ubora.
“Simamieni wakandarasi vizuri katika kutekeleza ujenzi wa miradi hii. Msisimamie kwa mazoea, bali kwa weledi na kasi ili tija ya miradi hii ionekane na wananchi wapate huduma kwa wakati,” amesema Twange.
Pamoja na kutoa maagizo hayo, Twange amewapongeza wasimamizi kwa hatua zilizofikiwa licha ya changamoto zilizopo, akisisitiza umuhimu wa kutumia kipindi hiki kisicho na mvua kufanya kazi kwa kasi zaidi.
Vilevile, Twange ametembelea miradi ya upanuzi wa vituo vya Cotex (Iringa) na Makambako (Njombe) ambavyo tayari vimekamilika kwa kiasi kikubwa na vimeanza kutoa huduma kwa wateja, jambo linaloongeza uimara wa upatikanaji wa umeme katika mikoa hiyo.
“Nimefurahishwa na utekelezaji wa miradi hii ya vituo vya kupoza umeme katika mikoa ya Iringa na Njombe. Kwa sasa tuna uwezo mkubwa wa kuhudumia wateja wengi zaidi kuliko hapo awali,” amesema Twange.
Mradi wa Taza ni sehemu ya juhudi za Tanzania kushiriki kikamilifu kwenye soko la kikanda la umeme kupitia Southern Africa Power Pool (SAPP), namradi huu utaongeza usalama wa upatikanaji wa umeme na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Twange pia alitembelea miradi mingine ya umeme inayotekelezwa mkoani Iringa, ikiwemo ya upanuzi wa njia za kusafirisha umeme na vituo vya kupozea umeme.
Mradi wa Taza unafadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na taasisi za fedha za kimataifa zikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida).

Katika ziara hiyo, Tanesco pia iliendeleza kampeni yake ya “Umeme ni nishati nafuu zaidi jikoni” kwa kukabidhi majiko yanayotumia umeme mdogo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, na Katibu Tawala wa Mkoa, Doris Kalasa.
Twange amesisitiza umuhimu wa matumizi ya umeme kama nishati safi kwa matumizi ya majumbani, hasa kwa kupikia, akisema kuwa lengo ni kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao unaharibu mazingira.
“Tunawaomba viongozi waendelee kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi. Umeme ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amepongeza juhudi za Tanesco na kueleza kuwa hali ya upatikanaji wa umeme mkoani humo imeimarika na kuleta tija kwa wananchi.
“Hali ya umeme sasa ni ya kuridhisha. Tumeona jinsi ambavyo huduma imeboreshwa na Tanesco wanatoa taarifa kwa wakati na ushirikiano ni mzuri,” amesema James.
Aidha, Katibu Tawala wa Mkoa, Doris Kalasa amesisitiza umuhimu wa wananchi kuelimishwa kuhusu matumizi bora ya nishati ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.