Mabingwa watetetzi wa Kombe la CHAN, Senegal wameanza vibaya maandalizi ya michuano hiyo baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 katika mashindano ya CECAFA Pre CHAN dhidi ya Uganda.
Katika mchezo huo uliofanyika leo Julai 24, 2025 kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu mkoani Arusha, timu hizo zilienda mapumziko zikiwa hazijafungana.
Baada ya kurejea kipindi cha pili, dakika ya 64 Arnold Odong akaitanguliza Uganda, kisha dakika tatu baadaye Kanande Patrick akapachika la pili kwa mkwajiu wa penalti.
Senegal ilicheza dakika 21 ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi ilipofika dakika ya 88 na kupata la kufutia machozi lilofungwa na Sergine Moctar.
Senegal ilifika Karatu jana kwaajili ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya Uganda na Tanzania kabla ya kuanza kwa CHAN 2024 itakayofanyika nchi za Tanzania, Uganda na Kenya kuanzia Agosti 2 hadi 30, 2025.
Wakati wa kuwasili, Kocha Mkuu wa Senegal, Souleymane Diallo alisema ana furaha kubwa kwamba timu yake itacheza mechi mbili za kirafiki katika Mashindano ya CECAFA Pre-CHAN kwani itampa mwanga mzuri wa kujua ubora na upungufu uliopo kabla ya kuanza kwa safari ya kutetea taji lao.
“Mechi hizi mbili zitakuwa muhimu sana kwa timu yangu tunapojiandaa kujaribu kutetea taji la CHAN mwezi ujao. Kila mechi ya ushindani ambayo timu inacheza inasaidia sana kwa sababu hutusaidia kuboresha vipengele kadhaa,” alisema.
Katika kikosi hicho, Senegal itakuwa na Serigne Moctar Koité ambaye ni mchezaji pekee aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda ubingwa wa CHAN 2023 ikiifunga Algeria kwenye fainali.
Senegal, ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la CHAN, baada ya leo kucheza na Uganda, Jumapili wiki hii itaikabili Tanzania kwenye Uwanja wa Black Rhino mjini Karatu kuanzia saa 9:00 alasiri.
Senegal ipo kundi D katika michuano ya Chan 2024 pamoja na Nigeria, Congo Brazzaville, na Sudan ambapo mechi zao zitachezwa Zanzibar.
KIKOSI CHA SENEGAL KILICHOKUJA KWAAJILI YA CHAN
Makipa: Idrissa Ndiaye, Samba Mballo, Marc P.A. Diouf
Mabeki: Seyni Mbaye Ndiaye, Mbaye Ndiaye, Amadou Bene Coly, Layousse Samb, Malick Sembène, Baye Assane Ciss, Daouda Ba
Viungo: Ousseynou Fall Seck, Moussa Cissé, Bonaventure Fonseca, Serigne Moctar Koité, Mbaye Yaya Ly, Insa Boye, Issa Kane, Pape Abasse Badji
Washambuliaji: Mapathé Mbodji, Libasse Gueye, Christian Gomis, Oumar Ba, Vieux Cissé, Ababacar Sarr, Ameth Niang