Uvumi kuhusu kuonekana viungo vya binadamu Magole, Polisi yaonya wahusika

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayohusisha mabaki ya viungo vya binadamu kudaiwa kukutwa eneo la Magole Mpiji Dar es salaam, ni tukio la miaka 11 iliyopita.

Jeshi hilo kupitia taarifa iliyoitoa leo Julai 24, 2015, limesema tukio hilo ufafanuzi wake ulitolewa Julai 22, 2014 na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam wakati huo.

“Jeshi la Polisi Dar es salaam linapenda kuwatoa hofu wananchi juu ya taarifa yenye lengo la kutengeneza taharuki katika jamii kuhusiana na mabaki ya viungo vya binadamu kudaiwa kukutwa eneo la Magole Mpiji Dar es salaam, taarifa ya tukio hilo ni ya zamani miaka 11 iliyopita,” imeeleza taarifa ya Polisi.

Kutokana na tukio hilo kwa wakati huo, jeshi hilo limesema watu wanne wakiwemo madaktari na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) kilichopo Kunduchi Dar es Salaam, walikamatwa.

Wataalamu hao wakati huo walikamatwa baada ya uchunguzi uliohusisha Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya na mamlaka zingine za kiuchunguzi.

“Kukamatwa kwao kulitokana na taarifa za wananchi zilizopatikana kuwa katika bonde la Mto Mbezi eneo la Magole Mpiji, Kinondoni, kulikuwa na viungo mbalimbali vya miili ya binadamu,” imeeleza taarifa hiyo.

Baada ya Polisi kufika eneo lile na uchunguzi kufanywa kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali, ilibainika viungo vile vya binadamu vilikuwa vimetolewa kwenye maabara ya mafunzo ya chuo cha IMTU na kwenda kutupwa eneo lile kinyume na sheria au utaratibu, baada ya kuwa vimetumika kwenye mafunzo kwa vitendo katika chuo hicho,” taarifa ya Polisi imeeleza.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa wahusika wakiwemo madaktari wataalamu wa chuo hicho walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni wa wakati huo Kwey Rusema na Wakili wa Serikali Magoma Mtani.

Wataalamu hao walisomewa mashitaka kuhusiana na suala hilo la kutupa viungo hivyo eneo lile.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linaendelea kuwatahadharisha watu wenye tabia ya kutoa taarifa zenye malengo ya kuzusha taharuki na kujenga hofu kwa umma kuwa, halitasita kuchukua hatua za kisheria juu ya tabia hizo,” imeonya taarifa hiyo ya Polisi.