Wadau wafunuka wasiwasi Sowah kutua Simba

Wakati Simba ikiripotiwa kuwa mbioni kumnasa Jonathan Sowah wa Singida Black Stars, Wachambuzi na makocha wa soka wameonyesha wasiwasi juu ya tabia za utovu wa nidhamu kwa nyota huyo ingawa wanaamini ni mshambuliaji sahihi kwa Wekundu hao wa Msimbazi.

Sowah ambaye amefunga mabao 13 katika mechi 13 alizoitumikia Singida Black Stars tangu alipojiunga nayo katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari mwaka huu.

Kocha wa soka na mchezaji wa zamani wa KMKM, Ibrahim Masoud ‘Maestro’ alisema kwamba Sowah anapaswa kubadilika kinidhamu ili aisaidie Simba.

“Unaweza ukawa na matukio mengine kama vile nidhamu yako ni mbovu lakini bado kipaji chako kikawa kinaendelea kuzungumza. Mara nyingi katika dunia ya leo wachezaji hao wapo. Mimi sipendi tabia za utukutu ambao umepitiliza, wachezaji ambao mara nyingi wanasababisha timu kuwa pungufu kwa kupata kadi.

Huyu (Sowah) ni mmoja kati ya wachezaji wazuri sana katika bara hili la Afrika ambaye kila mmoja anatamani kuwa naye. Sina shaka na uwezo wake ndani ya mchezo. Mashaka yangu yapo sehemu moja tu ambayo ni nidhamu ya mchezo. Endapo atakwenda kwenye klabu kama Simba na akatimiza malengo yake kama mchezaji basi ni msaada mkubwa sana kwa timu na Simba itakuwa imepata mshambuliaji mzuri sana.

“Hakuna shaka na uwezo wake ni suala la akili tu. Kuibadilisha itoke ajue anaenda kucheza katika timu nyingine kubwa, ina wafuasi wengi na hisia kubwa za soka. Natamani kumuoana akigezua akili yake na natamani kumuona akiishi kama mchezaji wa kulipwa,” alisema Maestro.

Mchambuzi wa soka, Edo Kumwembe amesema kuwa anaamini Simba itakuwa imeamua kuweka kipaumbele zaidi ubora wa Sowah kuliko suala la nidhamu yake.

“Simba wakimpata Sowah watakuwa wanaiimarisha timu yao kwa kiasi kikubwa sana na watakuwa wanarudisha makali ya John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu ambao tangu walipoondoka hakuna mshambuliaji aliyeweza kuvaa viatu vya angalau mmoja kati yao. Namba za Sowah zinajieleza.

“Watu wanajiuliza kuhusu nidhamu lakini kwa wenzetu hawawezi kumuacha mchezaji mzuri kwa sababu ya nidhamu. Mabao yake ni muhimu kuliko nidhamu na wanaamini wanaweza kumrekebisha,” alisema Kumwembe.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Said Maulidi ‘SMG’ amesema Sowah ameonyesha uwezo mkubwa ndani ya muda mchache huku akitaja nidhamu kuwa ndio shida inayomuangusha akimfananisha na Mario Balotelli.

“Ubora aliouonyesha unaweza ukawa ni uwezo wake binafsi au amebebwa na timu anayoichezea. Nafikiri ni mtu sahihi lakini watafute mtu wa kukaa naye ili kumjenga apunguze hasira au nidhamu mbovu inayosababisha kuiangusha timu kutokana na adhabu zake za mara kwa mara za kadi nyekundu.

“Sowah ukiondoa mchezo wa fainali kombe la Shirikisho, tulicheza naye mechi ya kimataifa pia alionyeshwa kadi lakini kabla ya mchezo wetu huo wa kimataifa alikuwa ametoka kukosa mchezo kutokana na kadi nyekundu hivyo ni mchezaji ambaye anaiangusha timu kwa shida zake binafsi,” alisema SMG.

Meneja wa Singida Black Stars, Hamis Tamwbe amesema kuwa Sowah ni mshambuliaji mzuri.

“Mechi 13 amefunga mabao 13 unajiuliza angeanza msimu angekuwa na mabao mangapi kwenye mechi zilizobaki akifunga bao kwenye kila mchezo? Anajua kucheza nma akili za mabeki lakini pia analijua goli,” alisema Tambwe.