Morogoro. Ikiwa imepita miezi minne tangu kutokea kwa tukio la ajali ya moto uliounguza karakana na vibanda 16 vya kutengeneza na kuuza samani za ndani, Mtaa wa Ngoto Manispaa ya Morogoro waathirika wa tukio hilo wameanza upya biashara wakitumia vifaa na mashine duni.
Mafundi selemala na wafanyabiashara hao wamelazimika kutumia vifaa na mashine hizo duni ambazo ni za kizamani baada ya mashine za kisasa za kutumia umeme walizokuwa wakitumia awali.
Tukio hilo lililotokea Aprili 21 mwaka huu majira ya usiku, taarifa ya uchunguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji imeeleza chanzo cha moto huo ni kishungi cha sigara kilichotupwa kwenye takataka za randa na mtu ambaye hajafahamika mpaka sasa.
Leo Julai 24, Mwananchi ilifika katika eneo hilo la kutengeneza na kuuza samani kwa lengo la kuona hali ya biashara hiyo baada ya tukio hilo la moto, hata hivyo imeshughuhudia mafundi wakitumia randa, misumeno na vifaa vingine ambavyo wamekuwa wakifanyia kazi kwa kutumia nguvu.
Aidha Mwananchi imeshuhudia bidhaa za samani za ndani vikiwemo vitanda makabati na milango zikipigwa na jua, baada ya banda lililokuwa likitumiwa na wafanyabiashara hao kuhifadhi na kuuzia samani hizo kuungua moto na wafanyabiashara hao kushindwa kujenga tena banda hilo.
Akizungumzia hali ya biashara tangu lilipotokea tukio hilo, Mwenyekiti wa umoja wa mafundi na wafanyabiashara wa samani katika eneo hilo Shukuru Magari amesema wameshindwa kujenga tena banda la kuuzia samani kwa sababu kwa sasa hali zao kiuchumi ni mbaya, hasa baada ya kupoteza mitaji huku wengine wakiwa na madeni kwenye benki na taasisi mbalimbali za kifedha.
“Baada ya tukio lile la moto wengi wetu tumeyumba kiuchumi na wengine wamepoteza mitaji maana bidhaa zote ziliteketea kwa moto, mashine na katakana nazo ziliteketea, hivyo sasa ndio tumeanza upya kuinuka, na ndio maana unaziona hizo bidhaa hapo juani na hata ikitokea mvua basi zitanyeshewa kwa sababu hatuna sehemu nyingine ya kuzihifsdhi,” amesema Magari.
Amesema kitendo cha kutumia mashine za kizamani kumekuwa kukiwafanya wachoke kwa sababu wanatumia nguvu nyingi na pia kitendo cha kuweka bidhaa zao juani kimekuwa kukipunguza ubora wa bidhaa hizo.
Magari amesema tathimini ya awali inaonyesha hasara waliyoipata kutokana na tukio hilo la moto kwa ujumla wao ni zaidi ya Sh100 milioni na kwamba kutokana na hasara hiyo wapo baadhi ya wafanyabiashara mpaka sasa hawajaweza kupata mitaji, na hivyo kwa sasa wamekuwa wakifanya kazi kwa wenzao.
“Wapo wenzetu kama watano hivi ambao baada ya tukio lile la moto hawakuweza kuinuka tena kibiashara, kwa ufupi hawana mitaji na hivyo tuko nao hapa tumejibanza pamoja ili mradi nao inapofika jioni waweze kurudi nyumbani wakiwa na chochote mkononi ili watoto wapate rizki.
“Sisi wengine ndio tumerudi kwa kujikongoja huku tukitumia zana na vifaa vya kizamani walivyofanyia kazi babu zetu hata hivyo bado kazi ni ngumu, samani ambayo ilikuwa ikitengenezwa kwa siku mbili sasa hivi tunatengeneza kwa siku nne hadi wiki,” amesema Magari.
Akieleza madeni ya benki wanayodaiwa Magari amesema tayari mazungumzo yanaendelea kufanyika kati yao na benki hizo ili kuona namna madeni hayo watakavyolipa bila kuathiri mitaji yao ambapo amesema umoja wao una wanachama zaidi ya 200 na wote wamekuwa wakichukua mikopo kwenye mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha.
Pamoja na changamoto hizo, magari amewashukuru viongozi mbalimbali kuanzia Serikali ya mtaa hadi mkoa kwa kuwakimbilia na kuwapa msaada wa hali na mali.
“Miongoni mwa viongozi hao waliotukimbilia ni pamoja na mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini AbdulAziz Abood na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala ambaye yeye alitupa msaada wa bati 162 ambazo tuligawana na kuweza kila mmoja kujenga katakana yake japo ndogo kwa ajili ya kufanyia kazi,” amesema Magari.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amewaomba wadau wengine kuwashika mkono ili waweze kurudi kwenye hali ya awali ambapo ametaja baadhi ya vitu ambavyo wanaomba kusaidiwa kuwa ni pamoja na mashine na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi ambayo vinatumia umeme ili waweze kuondokana na vifaa na mashine duni za kizamani, lakini pia kwa niaba ya wenzake ameomba wapatiwe msaada wa kujengewa banda kwa ajili ya kuhifadhi na kuuzia bidhaa zao.
Magari amesema kingine wanachoomba ni kupatiwa mikopo ya Halmashauri ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ili waweze kuinuka kibiashara.
“Hii mikopo inayotolewa na Halmashauri ya asilimia nne kwa vijana, asilimia nne kwa wanawake na asilimia mbili kwa wenye ulemavu nimeshawahi kusikia lakini kiukweli bado sijajua nawezaje kuifuatilia mpaka tupate, hivyo kama tutapata mtu wa kutushika mkono na kutuelekeza hatua kwa hatua ili tupate hii mikopo tunashukuru,” amesema Magari.
Naye mwanachama wa umoja huo wa mafundi selemala na wafanyabiashara wa samani Hussein Ally amesema changamoto nyingine kubwa wanayopata ni madeni ya wateja ambao samani zao ziliungua moto kabla ya kukabidhiwa.
Ally amesema wamekuwa wakiendelea kuwalipa baadhi ya wateja kidogo kidogo fedha zao ama samani walizonunua hivyo kwa sasa muda mwingi wamekuwa wakitumia kutengeneza samani za kuwalipa wateja.
“Kwenye hii biashara yetu wapo wateja wanaokuja kununua samani ambazo tayari tumeshazitengeneza, lakini pia wapo wateja ambao wanakuja na picha ya samani wanazotaka na aina ya mbao wanayotaka, kwa sasa ndio tunawalipa madeni ya wateja hao kwa sababu wapo ambao walishalipa fedha yote ya gharama ya hizo samani, Sasa kazi tuliyonayo ni kulipa madeni na wakati huo huo kutengeneza samani za kuuza ili maisha yaendelee,” amesema Ally.
Amesema ajali hiyo ya moto kwake yeye imemuathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu hakuweza kuokoa chochote na samani nyingi zilizoteketea ni zile ambazo tayari alishachukuwa fedha kwa wateja ikiwemo milango, vitanda na makabati.
Fundi na mfanyabiasha huyo amesema mbali na kudaiwa na wateja lakini pia kwa umoja wao wamekuwa wakidaiwa kodi ya eneo wanalofanyia biashara hiyo.
Akieleza mikakati ya kuzuia majanga ya moto na mengine Ally amesema kwa sasa wamekuwa wakichukua tahadhari kwa kufanya usafi wa mara kwa mara kuzunguka eneo la katakana na kuzuia matumizi ya sigara kwa wao wenyewe na watu waliopo jirani na eneo hilo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala amewataka wafanyabiashara hao kufuata utaratibu ili waweze kupata mikopo ya Halmashauri ambayo kwa kiasi fulani itaweza kuwasaidia katika shughuli zao.
Mbali ya mafundi pamoja na wafanyabiashara wengine walioathirika na tukio hilo ni mwanamke mmoja Teddy Antony ambaye nyumba yake ilikuwa jirani na eneo hilo ambayo iliungua na kuteketea kabisa bila ya kuokoa chochote.