WANAOFANYA BIASHARA MTANDAONI BILA KUJISAJILI TRA WAPEWA MWEZI MMOJA KUJISAJILI

:::::::::

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda, ametoa wito kwa wafanyabiashara wa mitandaoni ambao hawajajisajili na TRA kujisajili mara moja ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Ameyasema hayo wakati akizindua rasmi utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya TRA na Shirika la Kimataifa linashughulika na masuala ya Kodi (IBFD) ambao umefanyika katika Chuo cha Kodi (ITA) jijini Dar es Salaam Leo tarehe 24.07.2025.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema wametoa mwezi mmoja kuanzia Agosti Mosi mpaka Agosti 31.2025 wafanyabiashara wote wanaoendesha shughuli zao mtandaoni wajisajili TRA ili waanze kuchangia katika kulipa Kodi wakiwemo wenye nyumba wanaopangisha nyumba zao kutumia Air BNB na hawalipi kodi.

Amesema watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo la kujisajili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja watachukuliwa hatua ikiwemo kutozwa faini maana hawajasamehewa kulipa kodi hiyo wakiwemo wale wanaouza vitu mbalimbali mtandaoni bila kulipa kodi kwani wanavunja sheria kwa kutokulipa kodi hiyo.

“Kuanzia Agosti Mosi tutakuwa na kampeni kubwa ya kuhakikisha kila anayefanya biashara ya kupangisha nyumba kupitia mtandao anasajiliwa na kulipa Kodi pamoja na watu wanaofanya biashara mtandaoni ambao kipato chao kinazidi Sh. 4,000,000 kwa mwaka nao watatakiwa kulipa Kodi na kila mmoja atalipa kutokana na kipato chake” amesema Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda ametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za watu wanaofanya biashara mtandaoni kuziwasilisha TRA na kuwa zipo njia nyingi za kuwabaini watu ambao hawalipi kodi hata kama wanafanya biashara mtandaoni na risiti zitatolewa kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa VFD.

Amesema ufuatiliaji wa biashara mtandao utawezeshwa na mafunzo ambayo watumishi wa TRA wamepatiwa kwa ushirikiano na IBFD kwa udhamini wa Serikali ya Uholanzi na kubainisha kuwa makampuni yaliyowekeza nchini na kujihusisha na ukwepaji wa kodi yatafikiwa.

Mwenda amesema Serikali ya Tanzania imefungua milango ya uwekezaji ambapo makampuni mengi yanakuja kuwekeza hivyo yanao wajibu wa kulipa Kodi kwa Mujibu wa sheria.

 = = = = = = =