Watatu waagwa,  kwenda kuliamsha ANOCA Algeria

TANZANIA itawakilishwa na wanamichezo watatu katika mashindano ya kwanza ya Kamati za Olimpiki za Kitaifa za Afrika (ANOCA).

Mashindano hayo yatafunguliwa Jumamosi ya Julai 26 huko Algiers, Algeria.

Katika mashindano hayo, Tanzania itawakilishwa na wanariadha wawili, 
Grace Charles na Baraka Sanjigwa sambamba na mchezaji mmoja wa tenisi ya meza, Qutbuddin Taherali.

Timu ya riadha itaongozwa na kocha Robert Kalyahe, huku upande wa tenisi ya meza timu itakuwa chini ya kocha Masoud Mtalaso.

Wanamichezo hao wameondoka nchini jana kwenda Algeria tayari kwa michuano hiyo mikubwa ya nchi mwanachama wa Olimpiki kwa ukanda wa Afrika.

Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid amesema  wanamichezo hao ni miongoni mwa wanafunzi wa Shule za Sekondari waliowika katika mashindano ya Shule za Sekondari (UMISSETA) yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Iringa.

  “Hili ni tukio la kihistoria, tuna matumaini watafanya vizuri kwenye mashindano,” alisema Gulam wakati akiikabidhi timu hiyo  bendera ya taifa.

Aliongeza Watanzania wanatarajia kuwaona wakifanya vizuri na kuipeperusha vema bendera ya taifa.

Kwa upande wa kocha Kalyahe, alisema  maandalizi yamefanyika kwa kiwango kizuri na wanatarajia matokeo mazuri.

 Akifafanua ushiriki wa Tanzania katika riadha, Kalyahe amesema Baraka atashiriki mbio za mita 100 na 200, huku Grace akishiriki mbio za mita 200 na 400.

 “Tumefanya mazoezi ya kutosha, tunashukuru TOC (Kamati ya Olimpiki Tanzania?  Kwa kufanikisha safari hii, pia tunaishukuru serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kuisaidia timu yetu.

“Tuna jukumu moja tu nchini Algeria, kuiwakilisha vema Tanzania,” amesema Kalyahe.

Afisa michezo mwandamizi kutoka BMT, Charles Maguzu, pia aliwataka wanamichezo hao kujitahidi na kufanya vizuri katika mashindano hayo. 

Timu hiyo itaongozwa na Nasra Juma ambaye ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya TOC na ndiye mkuu wa msafara huo.