Watatu wakalia kuti kavu Mashujaa FC

UONGOZI wa maafande wa Mashujaa, huenda ukaachana na nyota watatu wa kikosi cha kwanza msimu huu, baada ya kutokuwa na maelewano mazuri ya kuongeza mkataba mpya, huku mabosi wa timu hiyo wakiendelea kupambana kwa lengo la kubakia nao.

Nyota wanaotajwa huenda wakaachana na timu hiyo ni beki wa kulia, Omary Kindamba, beki wa kati, Ibrahim Ame na kiungo wa ukabaji, Zubery Dabi, ambao wote mikataba yao imeisha, japo mabosi wa kikosi hicho wanapambana kuhakikisha wanabaki nao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika alisema wanaendelea kupambana kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho ili kilete ushindani msimu ujao, huku wakianza pia mazungumzo ya kuongezea mikataba nyota wote waliomaliza.

“Wakati tunapambana kuboresha kikosi chetu kwa kuongezea nguvu wapya, pia tunaendelea kuwaongezea mikataba wengine waliomaliza, taratibu hizo zimeanza na hadi kufikia Agosti 1, 2025, nafikiri tutajua kitakachotokea,” alisema Meja Tika.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua huenda mastaa hao wakaachwa baada ya kumrejesha aliyekuwa beki wa kati wa timu hiyo, Samson Madeleke aliyetokea Pamba Jiji, huku ikimsajili pia kiungo, Samwel Onditi kutoka Kagera Sugar iliyoshuka daraja.

Mbali na nyota hao, wengine waliosajiliwa ni aliyekuwa winga wa KenGold, Selemani Bwenzi na mshambuliaji, Salum Kihimbwa kutokea Fountain Gate na tayari wamekamilisha taratibu za kutua katika kikosi hicho kwa mikataba ya miaka miwili.