Watoto wenye umri wa miaka 13 waweka rekodi kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro

Moshi. Ibrahimu Elias (13) na Specioza Erasto (13) ambao wanalelewa katika kituo cha watoto yatima cha Moyo wa Huruma mkoani Geita wameweka historia ya kufika katika kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro ambao ndiyo mlima mrefu kuliko yote barani Afrika.

Watoto hao ambao wanasoma darasa la saba katika shule ya msingi Mbughani iliyopo mkoani humo, wameshuka leo Julai 24, 2025 kupitia lango la Mweka wilayani Moshi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya GGM Kili Challenge 2025, inayodhaminiwa na kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids).

Julai 18, 2025, tukio hilo liliwakutanisha wapanda mlima 49 na waendesha baiskeli 17 kutoka ndani na nje ya nchi ambao walizunguka hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuchangisha fedha na kuongeza uelewa kuhusu mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi nchini.

GGM Kili Challenge imelenga kukusanya Dola za Kimarekani milioni moja kila mwaka, kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Wakizungumza mara baada ya kushuka Mlima Kilimanjaro, watoto hao wameonyesha furaha yao huku wakisema walikuwa wakisoma mlima huo kwenye vitabu na wakati mwingine kuuona kwenye runinga.

Specioza, ambaye analelewa katika kituo hicho, amesema anajivunia kuweka historia ya kupanda mlima huo huku akisema ni historia ambayo haitafutika katika maisha yake.

“Najivunia kupanda Mlima Kilimanjaro, ni mlima mzuri lakini kitu kilichonifurahisha Zaidi, kuna uoto mzuri wa asili, namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupanda na kufika kilele cha uhuru,” amasema mwanafunzi huyo.

Ameongeza kuwa: “Furaha yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro ni kutengeneza historia yangu, nilivyokuwa nausikia, nilikuwa naona ni vigumu sana kupanda lakini nilivyopanda na kushuka salama, nimefurahi na kuona ni jambo la heri,” amesema mwanafunzi huyo.

Kwa upande wake, Ibrahimu amesema Mlima Kilimanjaro unavutia na hakutegemea kuona mlima huo ukiwa na maua mazuri ya kuvutia kama ulivyo.

“Namshukuru Mungu kwa mara ya kwanza nimepanda Mlima Kilimanjaro na kufika kileleni, najisikia vizuri sana, nimependa mazingira yalivyo mazuri na maua mazuri, mwaka kesho nitatamani kupanda tena,” amesema.

Aidha, amewataka watoto wenzake kupanda mlima huo kwa kuwa una historia nzuri na yenye kuvutia, hasa pale unapofanikiwa kufika katika kilele hicho cha mlima.

Akizungumzia watoto hao kufika katika kilele hicho, mratibu wa masuala ya Ukimwi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Adela Mpina amasema watoto hao kufika katika kilele cha mlima huo sio jambo jepesi, ni ujasiri unaopaswa kuigwa kwa wazalendo wa nchi hii.

“Sio jambo jepesi kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro, lakini vijana wetu wa wamekuwa tayari na wameonyesha uwezo mkubwa katika kujiamini, ujasiri, hata sisi wenyewe wanapoondoka kwenda kupanda, tulikuwa tuna hofu kutokana na umri wao,” amesema Adela.

Pamoja na mambo mengine ameipongeza kampuni ya GGML kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kutokea Virusi vya Ukimwi na Ukimwi nchini.

“Mchango wa GGML ni mkubwa katika mapambano haya ya Ukimwi na wameungana na Tacaids kutengeneza zile afua zinazohusiana na masuala ya Ukimwi, Serikali inadhamini sana mchango wao,” amesema Adela.

Naye, Makamu wa Rais wa Uendelevu na Uhusiano Africa, Anglo-Gold Ashanti, Simon Shayo amesema uwepo wa kampuni ya GGML hapa nchini umeleta mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

“Leo tumepokea wenzetu waliopanda Mlima Kilimanjaro lengo ikiwa ni kupaza sauti uwepo wa Virusi vya Ukimwi na Ukimwi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano haya,” amesema Shayo.

Ameongeza kuwa: “Mwaka huu tunafikisha miaka 25 ya mafanikio makubwa sana kupitia kampuni ambazo mpaka kufikia sasa tumesajiri watu 7,000 lakini tumekuwa ni wachangiaji wakubwa katika shughuli za kiserikali.”