Wawekezaji wa taasisi kutoka Tanzania, Kenya na Uganda wamekutana jijini Arusha kujadili jinsi ya kuhamasisha mitaji ya ndani katika uwekezaji kwenye sekta za nishati, maji, usafirishaji na miunganisho ya kidijitali.
Hatua hiyo inatajwa kama njia muhimu na ya haraka katika kusukuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi za Afrika Mashariki.
Jukwaa hilo limeandaliwa na Benki za Stanbic nchini Tanzania, Kenya na Uganda, lengo likiwa ni kuhamasisha mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi za ndani kuchukua nafasi kubwa katika kufadhili maendeleo ya kiuchumi ya ukanda huu.
Washiriki walijumuisha mifuko ya pensheni, taasisi za fedha za maendeleo, wakala wa usimamizi wa mitaji na wadau wa sekta binafsi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo lililofanyika leo Alhamisi, Julai 24, 2025, Makamu wa Rais wa Taasisi za Fedha wa Stanbic Bank Tanzania, amesema Afrika Mashariki ina mtaji wa kutosha kusaidia maendeleo yake, lakini inahitaji kufanya kazi kwa pamoja.
“Ni ukosefu wa miradi ya kuwekeza, ukosefu wa maandalizi ya kutosha, na wakati mwingine, kutokuwa na usawa katika taarifa na sera. Jukwaa hili linawaleta wadau muhimu kwa ajili ya kushughulikia vikwazo hivyo,” amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Mwandamizi – Nishati na Miundombinu wa Stanbic Bank Tanzania, Aboubakar Massinda, amesema sekta binafsi iko tayari kushiriki katika uwekezaji wa miundombinu kama mazingira ya sera na kifedha yataruhusu.
“Tunahitaji kuona sera zinazotabirika, utayari wa kugawana hatari, na mifumo ya zabuni yenye uwazi,” amesema na kuongeza: “Tunaona fursa kubwa katika nishati mbadala, miundombinu ya majisafi na miunganisho ya kidijitali.”
Githuku Mwangi, ambaye nio mshauri wa kifedha wa taasisi ya CPF Capital and Advisory Services, amesema jukwaa hilo limetoa nafasi ya kipekee kwa wadau wa sekta kujadili namna bora ya kubuni bidhaa za kifedha ambazo zinaweza kuhamasisha uwekezaji wa muda mrefu kutoka kwa wawekezaji wa ndani.
“Tunahitaji kutengeneza mfumo wa bidhaa za kifedha zinazoshughulikia hatua zote – kuanzia fedha za awali za daraja, hadi mikopo ya muda mrefu inayofaa kwa miundombinu,” amesema.
Jonathan Muga, ambaye ni Makamu wa Rais Mwandamizi – Nishati na Miundombinu wa benki ya Stanbic Kenya, amesema wakati Serikali za Afrika Mashariki zinaendelea kushughulikia majukumu mengi, ni muhimu kwa sekta binafsi kuibuka kama mshirika imara katika maendeleo ya miundombinu.
“Serikali peke yake haziwezi kutekeleza miradi yote inayohitajika. Tunahitaji mtazamo wa pamoja wa sekta binafsi na taasisi za umma – siyo tu kwa ajili ya ufadhili, bali pia kwa ajili ya uendelevu na ufanisi wa utekelezaji,” amesema.
Naye Aime Uwase, ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango – Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema jukwaa hilo linaendana moja kwa moja na vipaumbele vya maendeleo vya EAC, ikiwa ni pamoja na Mpango wa Maono 2050.
“Jumuiya ya Afrika Mashariki inathamini nafasi ya sekta binafsi katika kutekeleza ajenda ya maendeleo ya kikanda. Miradi ya kipaumbele kama reli ya kisasa, usafiri wa anga wa kikanda, na nishati safi inahitaji ushirikiano thabiti kati ya sekta zote,” amesema.
Washiriki katika jukwaa hilo walikubaliana kuwa hatua inayofuata ni kuanzisha kikosi kazi cha kikanda kitakachoratibu uanzishaji wa miradi ya miundombinu kwa kuzingatia sera za ndani, viwango vya hatari, na matarajio ya mapato ya wawekezaji.