Klabu ya Yanga imetangaza hatua kubwa ya mabadiliko ndani ya kikosi chake kuelekea msimu wa 2025/2026, kwa kuthibitisha kuachana rasmi na wachezaji wake nyota watano, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya maboresho ya kikosi hicho kuelekea mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka klabuni, wachezaji hao hawatakuwa sehemu ya mipango ya kocha mpya Romain Folz, huku uongozi ukithibitisha kuwa tayari zoezi la usajili wa wachezaji wapya linaendelea kwa kasi.
Majina ya Waliotemwa:
Stephane Aziz Ki – Nyota huyu mahiri kutoka Burkina Faso ameuzwa rasmi. Alikuwa kiungo tegemeo wa timu na kipenzi cha mashabiki, lakini dili lake la uhamisho limekamilika kwenda Klabu ya Whydad Casablanca ya nchini Morocco.
Khalid Aucho – Kiungo wa Uganda aliyekuwa nguzo katika eneo la kati, naye hatakuwa sehemu ya kikosi kipya msimu ujao.
Clatous Chama – Staa kutoka Zambia ambaye aliwahi kung’ara pia akiwa Simba SC, naye ameondoka rasmi.
Kennedy Musonda – Mshambuliaji wa Zambia ambaye alionyesha uwezo mzuri msimu uliopita, lakini sasa anaagana na Wananchi.
Jonas Mkude – Kiungo mkongwe wa Tanzania aliyejiunga na Yanga akitokea Simba SC, naye hatakuwa sehemu ya kikosi cha msimu mpya.
Maboresho Yaendelea
Uongozi wa Yanga umesisitiza kuwa kuondoka kwa wachezaji hao ni sehemu ya mpango mpana wa kuijenga timu imara, yenye ushindani wa hali ya juu, hasa kwa kuzingatia mashindano ya kimataifa kama CAF Champions League.
Mashabiki wa Yanga sasa wanasubiri kwa hamu kutangazwa kwa majina ya nyota wapya watakaovaa jezi ya njano na kijani msimu ujao, huku wengi wakiweka matumaini yao kwa kocha Folz kuleta mfumo mpya wa kisasa.