Dar es Salaam. Mfanyabiashara Shafii Mkwepu(46) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh62 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Mkwepu amefikishwa mahakamani hapo leo, Julai 25, 2025 na kusomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Wakili wa Serikali, Frank Rimoy alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 18200/2025.
Wakili Rimoy alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda koa hilo kinyume na kifungu 301 na 302 cha Kanuni ya Adhabu Sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Mkwepu anadaiwa Januari 17, 2018 eneo la Goba, kwa nia ya kudanganya alijipatia fedha taslimu Sh60milioni kutoka kwa Pespicky Shayo kwa kumueleza kuwa atamnunulia kiwanja, kitu ambacho alijua sio kweli.
Shtaka la pili, mshtakiwa huyo anadaiwa Desemba 24, 2018 katika eneo la Goba, wilaya ya Ubungo, mshtakiwa alijipatia Sh2milioni kutoka kwa Respicky Shayo kwa madai kuwa atamsaidia kupima kiwanja hicho, wakati akijua kuwa sio kweli.
Shtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo, alikana mashtaka yake na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika.
Hakimu Nyaki alitoa masharti matatu ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo, ambapo mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria watakao saini bondi ya Sh5milioni kila mmoja.
Pia mshtakiwa anatakiwa kuwe dhamana ya fedha taslimu Sh31milion au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
“Sharti lingine, mshtakiwa hatakiwi kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam, mpaka kwa kibali maalum,” alisema Hakimu Nyaki.
Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 7, 2025 kwa kutajwa.