Arusha. Imeelezwa asilimia 95 ya vifo vya watoto wachanga nchini, husababishwa na kukosa hewa ya oksijeni wawapo tumboni au wakati wa kujifungua. Hayo yameelezwa na Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto nchini (PAT).
Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, Tanzania inasajili zaidi ya watoto milioni 2.3 wanaozaliwa hai kila mwaka. Hata hivyo, takriban watoto wachanga 51,000 hufariki dunia kila mwaka, huku wengine 43,000 huzaliwa wakiwa wafu na zaidi ya asilimia 87 ya vifo hutokea ndani ya wiki ya kwanza ya maisha.
Kutokana na hilo, PAT imeitaka Serikali na wadau kuwekeza zaidi katika vitengo vya huduma kwa watoto wachanga ili kupunguza kiwango kikubwa cha vifo vya watoto wachanga vinavyotokea kila mwaka nchini.
Rais wa PAT, Dk Theopista Masenge amesema hayo leo Julai 25, 2025 kwenye kongamano la pili la Afya na Ustawi wa Mtoto linaloendelea jijini Arusha.
Kongamano hilo limebebwa na kaulimbiu isemayo: “Ubora wa huduma: Kuwajengea uwezo wazazi kuhakikisha afya katika safari ya kila mtoto.”
“Tumegundua zaidi ya asilimia 95 ya vifo hivyo ni watoto kukosa hewa ya oksijeni wakiwa tumboni au wakati wa mama kujifunga,” amesema.
Dk Masenge amesema upatikanaji wa vitengo vya kisasa vya huduma kwa watoto wachanga ni suluhisho muhimu katika kupunguza vifo hivyo.
“Tunahitaji vitengo vya huduma ya watoto wachanga vilivyo na vifaa vya kisasa na wataalamu wa kutosha katika kila hospitali ya rufaa na hata ngazi ya mikoa na wilaya. Hii itasaidia kuokoa maisha ya maelfu ya watoto wanaozaliwa kila siku,” amesema.
Dk Masenge amesema wanalenga kuangalia huduma ya mtoto kuanzia kabla ya ujauzito, kipindi cha ujauzito, na wakati wa kujifungua.
“Wahudumu wengi wakipata maarifa haya itaisaidia si tu kupunguza vifo vya watoto, bali pia kupunguza watoto wanaozaliwa na mahitaji maalumu, wakiwemo njiti na utindio wa ubongo,” amesema.
Ripoti iliyochapishwa katika tovuti ya Umoja wa Mataifa Mei 10, 2023 iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) inasema kati ya watoto 10 wanaozaliwa, mmoja ni njiti na kila sekunde 40, mtoto mmoja kati ya hao hufariki dunia.
“Makadirio yanaonyesha kwamba mwaka 2020 takribani watoto milioni 13.4 walizaliwa kabla ya muda yaani njiti, huku karibu milioni moja kati yao wakifariki kutokana na matatizo yanayotokana na hali hiyo ya kuzaliwa kabla ya wakati,” ilisema taarifa hiyo.
UN ilisema kuzaliwa kabla ya wakati ndiyo sababu kuu ya vifo vya watoto, ikichukua zaidi ya kifo kimoja kati ya vitano vya watoto vinavyotokea kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano baada ya kuzaliwa.
Watoto njiti wanaonusurika wanaweza kukabiliwa na changamoto ya afya ya maisha yote na kuongezeka kwa uwezekano wa ulemavu na ucheleweshaji wa maendeleo.
Dk Masenga amesema changamoto kubwa kwa sasa wanayokabiliana nayo ni uhaba wa madaktari nchini.
“Tumesajili zaidi ya watoto milioni 2.3 wanaozaliwa hai kila mwaka, lakini nchini kuna madaktari bingwa wa watoto wasiozidi 350, hii ina maana kila daktari ahudumie watoto 100,000,” amesema na kuongeza:
“Hiki ni kiwango kikubwa sana, hivyo Serikali ione namna ya kuhakikisha kila hospitali ya mkoa inakuwa na madaktari bingwa wa watoto angalau wanne na hospitali ya wilaya inakuwa naye mmoja ili kuongeza wigo wa huduma za watoto na kuondoa vifo vya kusababishwa nchini,” amesema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amewataka madaktari hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, huku Serikali ikiendelea kutatua changamoto yao.
“Mfano changamoto ya uhaba wa madaktari, nikiri kweli upo lakini kuna maeneo wako wengi na mengine wachache kulingana na mahitaji halisi yaliyopo, hivyo kukifanyika uwiano tunaweza kuona uafadhali,” amesema.
Kongamano hilo lililoandaliwa na PAT kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, hufanyika kila baada ya miaka mitatu.