Moshi. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaack Amani amewataka Watanzania kuwa waangalifu kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 na kuwachagua viongozi wenye maadili na si waliojawa tamaa na ulafi wa madaraka.
Askofu Amani ametoa wito huo leo Julai 25, 2025 wakati wa maadhimisho ya jubilei ya miaka 100 ya Seminari ya Mtakatifu Yakobo Mtume, iliyopo Kilema Chini, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika seminari hiyo na kuhudhuriwa na maaskofu, mapadri, waseminari wa zamani na wa sasa pamoja na waumini wa kanisa hilo.
“Kristu alituonyesha mifano ya utumishi kwa kujitoa nafsi, Tanzania ya leo tunapata shida sana kwa baadhi ya viongozi ambao ubinafsi unawatafuna na ndio maana mali za pamoja zinaishia katika mifuko ambayo sio salama.
“Na sasa kwa sababu ya uchaguzi tuangalie sana, wale wenye ulafi ulafi tusiwachague hao kabisa,” amesema Askofu Amani na kuongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwachagua wale wanaojitoa kwa wengine bila ubaguzi na kujipendelea.

Mapadre kutoka sehemu mbalimbali waliosoma katika Seminari ya Mtakatifu Yakobo Mtume (St. James seminary) iliyopo kata ya Kilema chini, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, wakiwa kwenye maandamano kabla ya kuanza kwa ibada.
Amesema: “Wanaojitoa sadaka, wanaojali haki, usawa, wanaojali wadogo, maendeleo ya wote, hao ndio viongozi iwe ndani ya kanisa au nje ya kanisa, popote pale kiongozi anapoweka mahitaji ya raia mbele huyo ndiye anayefaa kuchaguliwa kuwa kiongozi.”
Kuhusu kusitishwa kwa misaada ya nje, Askofu Amani amesema nchi inapaswa kujiimarisha kutokana na utajiri uliopo na rasilimali zilizopo zinapaswa kugawanywa kwa usawa bila upendeleo.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ichi amesema kwa sasa baadhi ya Watanzania wamekumbwa na “ugonjwa wa uchawa” kwa viongozi waliopo madarakani, wakilenga kupata manufaa binafsi, jambo ambalo amesema halimpendezi Mungu.
“Tamanini ukuu lakini tambueni maana ya ukuu, ukuu wa kweli ni utumishi, na fundisho hilo ni muhimu sana, sio mnaousikiliza hapa, bali kwa Watanzania wote ambao tumepata ugonjwa wa kuwa chawa.
“Chawa wa kujikomba, wakujinadi, kujipenyeza kwa wale walio na madaraka kusudi na sisi tupate kitu, hayo hayatupeleki popote, yanatupeleka kwenye ushindani wa ovyo na huo ushindani haumpendezi Mungu,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Askofu Ruwai’chi amesema miaka 100 tangu kuanzishwa kwa seminari hiyo mwaka 1925, imeweka historia kwa kutoa viongozi wa dini wenye weledi ndani ya kanisa hilo.
“Katika miaka 100, wamepita vijana wengi hapa seminarini, wamepata malezi, wakapata fursa ya kupambanua miito yao, wengine wakawa mapadri na wengine wakaenda katika shughuli nyingine huko uraiani ambao tunawaita mapadri wa uraiani,” amesema Askofu Ruwai’chi.
Gombera wa seminari hiyo, Padri Pastory Mafikiri amesema seminari hiyo imetoa maaskofu 10, mapadri 625 na waumini walei wapatao 3,628.
“Wote walisoma katika seminari hii wanaikumbuka kama mlezi wao hodari kiroho kimwili na kitaaluma, malezi hayo yanaendelea mpaka sasa ambapo seminari yetu ina jumla ya waseminari 218,” amesema.
Amesema baadhi ya wanafunzi katika seminari hiyo wanashindwa kufikia wito wa upadri kutokana na mivuto mbalimbali ya usasa inayojikita katika maendeleo ya kiuchumi.