MABOSI wa Azam FC wanadaiwa wanaendelea kufanya mambo yao kimyakimya katika kuimarisha kikosi cha msimu ujao wa mashindano, wakidaiwa kwa sasa wapo katika mazungumzo na straika mmoja matata anayejua kufumania nyavu kutoka Afrika Kusini.
Azam ambayo hivi karibuni ilimtambulisha kocha mkuu mpya, Florent Ibenge kisha kushusha mashine kadhaa za maana, ikiwamo kumrejesha kiungo mkabaji wa zamani wa kikosi hicho aliyekuwa akicheza soka la kulipwa nchini Misri inadaiwa ipo mezani kwa sasa na straika wa zamani wa Kaizer Chiefs.
Straika huyo aliyekuwa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro ambaye ameitumikia pia siku za nyuma Marumo Gallants, ili kuiongezea nguvu timu hiyo.
Habari kutoka ndani ya Azam zinasema, klabu hiyo inamtaka Chivaviro aliyewahi kuwindwa na Yanga enzi za kocha Nasreddine Nabi kabla ya kocha huyo kutua Kaizer na kumsogeza akitokea Marumo iliyovaana na Yanga ya Nabi katika mechi za nusu fainali za Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023.
Lengo la kuchukuliwa kwa straika huyo mwenye umri wa miaka 32 ni kuimarisha kikosi cha Azam chini ya Florent Ibenge aliyetua hivi karibuni akitokea Al Hilal ya Sudan kutokana na kuondokewa kwa Alassane Diao, huku Mbrazili Jhonier Blanco akiwa mbioni kuuzwa Argentina.
Chivaviro aliyemaliza na mabao sita katika michuano ya CAF ya 2022-2023 nyuma ya Fiston Mayele aliyeibuka kinara na kuifikisha Yanga katika fainali iliyopoteza kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla ya sare ya 2-2 dhidi ya USM Alger ya Algeria akitua ataungana na Jephté Kitambala.
Taarifa za ndani kutoka katika klabu hiyo zinasema, mazungumzo kuhusu kumalizana na mchezaji huyo yamefikia pazuri na huenda akasaini mkataba wa miaka miwili ili kuungana na Kitambala anayesubiri kutambulishwa tu baada ya kunyakuliwa akitokea AS Maniema Union ya DR Congo.
Kwa sasa Chivaviro ni mchezaji huyu baada ya kuachana na Kaizer kwa kumaliza mkataba aliokuwa nao, huku akishindwa kufanya vizuri kiasi ya timu hiyo kumsajili Makabi Lulepo ambaye aliisaidia timu hiyo kubeba ubingwa wa Kombe la NedBank likiwa ni taji la kwanza baada ya kupitia miaka 10.
“Kama kila kitu kitafanyika tunavyokubaliana na mchezaji huyo, basi tutakuwa tumempata mchezaji mzuri atakayeongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Tunaendelea kufanya usajili kwa kusaidiana na kocha Ibenge, ndiyo maana kuna wachezaji wanaondoka kama Gibril Sillah ambaye alimaliza na mabao 11 na asisti mbili, inabidi asajiliwe mchezaji mwingine mwenye kiwango cha juu.”
Kilichoivuta Azam kuhitaji huduma ya mchezaji huyo anayetajwa kuwa na thamani ya Euro 200,000 kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Markt kwa Mei, 2025 ikiwa ni takribani Sh607 milioni.
“Mimi nipo Dar es Salaam kweli nimekuja kuzungumza na timu za huku kuhusu wachezaji wangu lakini kuhusu Chivaviro siwezi kusema chochote, ingawa lolote linaweza kutokea,” alisema Herve Tra Bi ambaye ni wakala wake.