Mbeya. Wakati bei ya ndizi mbivu ikipanda jijini Mbeya, wananchi waishio ndani na nje ya mkoa huo wametakiwa kuvumilia mabadiliko hayo kutokana na kuadimika kwa bidhaa hiyo kulikosababishwa na baridi iliyopo sasa.
Mbeya ni moja ya mikoa inayozalisha ndizi hasa katika Wilaya ya Rungwe ambapo kwa sasa imeonekana kuadimika sokoni na kufanya bei yake kupaa huku hali ya baridi ikitajwa kuathiri uzalishaji.
Muonekano wa ndizi mbivu katika soko la matunda na nafaka la Soweto jijini Mbeya. Nyingine baadhi ya wananchi wakikagua bidhaa hizo
Mwananchi limefika katika soko maarufu la Soweto jijini humo leo Julai 25, 2025 na kushuhudia uchache wa bidhaa hiyo ambayo kwa muda mwingine hutumika kama chakula au matunda kwa watumiaji.
Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wajasiriamali wa zao hilo wamesema kwa sasa ndizi mbivu zimekuwa adimu kutokana na hali ya baridi iliyopo kwa sasa na inapopatikana bei yake ni tofauti na iliyozoeleka.
Victoria Mgeja amesema hali ya hewa ya baridi imefanya bidhaa hiyo kupanda kulingana na ubora, kuanzia Sh500 hadi Sh3,000 tofauti na awali ilivyokuwa kati ya Sh500 hadi Sh2,000 kwa chane moja.
“Utakuta muda mwingine zimefubaa au zinaonyesha weupe, hii ni kwa sababu ya baridi, hizi zote tunatoa kule Tukuyu ambako ndio zinazalishwa zaidi, kwa hiyo baridi kule ni kubwa sana, ndio maana bei nazo zimepanda,” amesema Victoria.
Kwa upande wake, mkulima Bupe Luoga mkazi wa Kiwira, amesema kwa sasa uzalishaji wa zao hilo umepungua kutokana na hali ya hewa huku akieleza kuwa ni jambo ambalo hutokea ifikapo Julai hadi Septemba.

Muonekano wa ndizi mbivu katika soko la matunda na nafaka la Soweto jijini Mbeya. Nyingine baadhi ya wananchi wakikagua bidhaa hizo
“Hata ukija Kiwira, Tukuyu na njia yote hii ya Kyela, utaona ndizi zilivyopungua, hata shambani uzalishaji umekuwa mdogo na ni hali ya kawaida kwenye kipindi kama hiki cha baridi,” amesema Bupe.
Mwenyekiti wa soko hilo, Fredi Mwailongano amesema mabadiliko hayo ni ya kawaida kwa kila mwaka hasa inapofika kipindi cha baridi ndizi za aina hiyo kupotea na kupanda bei.
“Kwa maana hiyo, wale wanaofika Mbeya kwa mara ya kwanza au wanaokutana na mabadiliko ya bei, wawe wavumilivu, hiki ni kipindi cha baridi, kila mwaka hutokea hivyo,” amesema Mwailongano.
Ofisa Kilimo na Mifugo Wilaya ya Rungwe, Adam Salum amesema mabadiliko hayo hutokea kwa kipindi kutokana na hali ya uzalishaji. Ameeleza kuwa suala lingine ni kupanuka kwa biashara ndani na nje.

“Soko likipanuka, lazima bei ya bidhaa ipande, kuna baadhi ya magonjwa yanayoshambulia migomba na matumizi ya viuatilifu, pia, vinachangia kwa kiasi kidogo. Hivyo, hali yote hii inaweza kuleta mabadiliko.
“Kwanza hali hii inaongeza pia uchumi kwa wananchi, hata makusanyo katika halmashauri yamepanda kutoka Sh1 bilioni hadi Sh1.2 bilioni kutokana na miundombinu bora iliyowekwa na serikali,” amesema ofisa huyo.