ALIYEKUWA beki wa Simba Queens, Violeth Nickolaus ameshajiunga na kikosi cha FC Masar kinachoshiriki Ligi ya Wanawake huko Misri.
Violeth, aliyekuwa nahodha wa Simba Queens, aliondoka nchini juzi kujiunga na kambi ya timu hiyo inayoanza maandalizi ya mashindano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa kwa wanawake yatakayoanza mapema mwezi ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo alisema kuwa tayari amesaini mkataba wa miaka miwili na kuanzia sasa atatambulishwa rasmi.
“Ameshasaini tayari na aliondoka juzi kwenda kutambulishwa na kujiunga moja kwa moja. Nafikiri hadi leo atakuwa keshawasili Misri kumaliza taratibu nyingine,” alisema mtu huyo.
Kama Violeth atajiunga na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Misri, ataungana na Mtanzania mwenzake, Hasnath Ubamba, aliyekuwa kikosini hapo kwa misimu mitatu.
Nyota huyo wa timu ya taifa, Twiga Stars, alidumu Simba kwa takribani misimu minane na kuiwezesha timu hiyo kunyakua makombe manne ya Ligi ya Wanawake na moja la michuano ya CECAFA.