Mbeya. Ikiwa zimepita siku 17 tangu kijana Nature Wilson (18) kukwama na kukata tamaa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano hatimaye amerejeshewa tabasamu na kuondolewa katika malezi duni na kuanza safari ya elimu katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Uwata iliyopo jijini hapa.
Tabasamu hilo halijaishia kwa kijana Nature, pia mdogo wake Patrick Wilson (8) ameonyesha furaha baada ya kupata fursa ya kuanza elimu ya awali hadi darasa la saba katika Shule ya Msingi Uwata, jambo ambalo limevuta hisia kwa bibi mlezi Lucia Kapangala (65) kushindwa kujizuia na kuangua kilio.
Kilio cha Lucia kilivuta hisia ya mambo mawili ikiwepo upweka atakaopata baada ya wajukuu zake kuanza safari ya masomo, sambamba na kutuliwa mzigo wa malezi na makuzi ya watoto hao.

Imeelezwa watoto hao tangu wazaliwe hawamjui baba yao, huku mama yao Mzazi Lida Kapangala (34) ni mlemavu wa kusikia na hata uwezo wa kutambua chochote katika maisha ya kila siku.
Leo Ijumaa Julai 25, 2025 na Meneja wa Taasisi ya Tulia Trust Jackline Boaz chini ya Mkurugenzi wake Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson imefika nyumbani kwa watoto Nature (18) na Patrick (8) katika Mtaa wa Mwasote Kata ya Itezi jijini hapa na kuwachukua tayari kwa kaunza safari ya elimu.
Hatua hiyo imefuatia mwanzoni mwa Julai mwaka huu, Spika wa Bunge, Dk TuliaAckson kuliombwa na wananchi wa Mtaa wa Mwasote Kata ya Itezi kubebe jukumu la kuwasaidia kuuwasomesha watoto hao na kuitunza familia ya bibi yao Lucia Kapangala (65) ambao wanaishi mazingira magumu.
Awali, ilielezwa kijana Nature alihitimu elimu ya kidato cha nne Shule ya Sekondari Itezi na kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano Shule ya Sekondari Rungwe Wilaya ya Rungwe, mkoani hapa ambapo alikwama kutokana na kukosa mahitaji.
Hatua hiyo ilipelekea kukaa nyumbani kwa siku kadhaa huku akikata tamaa ya kupata elimu sambamba na mdogo wake Patrick ambaye alikuwa anasoma darasa la kwaza Shule ya Msingi Mwasote.
Lucia anasema licha ya watoto Nature na Patrick kuchukuliwa kuendelea na masomo kupitia Taasisi ya Tulia Trust bado yuko kaka yao ambaye yuko moja na Mkoa nchini akipambania maisha.

“Nimewalea kwa shida sana napika na kuuza pombe ili kumudu kutunza familia ya watoto wawili na Mama yao ,Lida Kapangala (34) ambaye ni Mlemavu wa kusikia na ajiwezi kwa chochote, “amesema.
Lucia amesema kimsingi wanaishi maisha duni na kuna wakati walala njaa kutokana na mfumo wa maisha ya kila siku.
Anasema kitendo cha Dk Tulia kuwachuka na kuwaendeleza kielimu ni cha kiungwana na kuwaombea safari yao ya elimu ikawe njema, lakini amewapa husia wakihitimu wakumbe kugusa jamii yenye uhitaji.
“Lakini nalia machozi ya furaha na huzuni kimsingi nitabaki mkiwa nilizoea kuishi na wajuku zangu sasa ni kama naanza safari mpya ya maisha,”amesema.
Akizungumza hatua ya kuwaendeleza kielimu, Meneja wa Taasisi ya Trust, Jackline Boazi amesema ni kufuatia maisha duni wanayopitia kwa kukosa chakula na mahitaji mengine hali inayopelekea kukosa utulivu wa kupata elimu.
Amesema hatua hiyo ni maelekezo ya Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo,kama muendelezo wa programu ya kusaidia wahitaji katika sekta ya elimu na kubainisha watakuwa chini ya uangalizi wa Taasisi hiyo.
“Kimsingi kama mlivyoona kijana, Nature (18) ameanza masomo Shule ya Sekondari ya Wavulana Uwata, lakini mdogo wake tumempeleka Shule ya Msingi Uwata ataanza elimu ya awali hadi darasa la saba,”amesema.
Katika hatua nyingine Jackline amesema kama Taasisi wametumia zaidi ya Sh5.8 milioni kwa ajili ya mahitaji mbalimbali zikiwepo sare za shule.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Uwata, Patrick Lalawima amesema ni jambo la kuishukuru taasisi hiyo na watahakikisha anafanya vizuri katika masomo.
“Kuna programu mbalimbali za masomo tutampitisha lengo ni kuona anatimiza ndoto zake za kupata elimu, lakini kupitia Dk Tulia siyo mwanafunzi wa kwanza kumleta shuleni hapa,” amesema.
Kwa upande wake kijana Nature amesema matarajio yake ni kufanya vizuri katika masomo na kuja kusaidia wahitaji wengine kwani kwake ni kama ndoto.