Mwanza. Zaidi ya washiriki 300 wanatarajiwa kushiriki kwenye kongamano la kitaaluma kuhusu nafasi ya ubia katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) jijini Mwanza.
Kongamano hilo linaloratibiwa kwa ushirikiano kati ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) litafanyika Julai 26, 2025 chuo cha Saut jijini Mwanza.
Washiriki, watoa mada na wajadili mada akiwemo mwanasiasa na mwanataaluma, Profesa Anna Tibaijuka watashindanisha hoja mbalimbali, kuzungumza na kupanua uelewa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Julai 25, 2025 katika chuo cha Saut jijini Mwanza, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya sayansi na siasa, Dk Lupa Ramadhani amesema kongamano hilo ni utekelezaji wa malengo ya dira ya maendeleo ambayo yanalenga kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
“Kwa hiyo tunataka tujadiliane kwa uwazi, kama mnavyofahamu wiki iliyopita tu Dira ya Maendeleo 2050 ilizinduliwa na Mheshimwa Rais (Samia Suluhu Hassan) Dodoma na msisitizo mkubwa umewekwa katika nafasi ya ubia na dira ile inataka kila Mtanzania kushiriki katika kuleta maendeleo ya nchi yake,” amesema Dk Ramadhani.
Amesema kutakuwa na mada kubwa tatu ikiwemo ya dhana ya PPP na nafasi yake kufikia Dira 2050, nafasi ya PPP katika kukuza uwekezaji na ufanisi katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa pamoja na nafasi ya sekta binafsi na mitaji kutoka nje katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania zitakazoendeshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, Dk Jasinta Msamula na Dk Delphine Kessy.
Pia, watakaojadili mada ni Profesa Tibaijuka, Dk Ponsian Ntui, Erastus Malai ambao ni washiriki kutoka serikalini na sekta binafsi pamoja na wananchi watashiriki kwa kutoa michango yao.
Hilo ni kongamano la pili, likiwa ni mwendelezo wa kongamano la kwanza lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mei, 2025 kabla dira hiyo kuzinduliwa.
Mkuu wa Kitengo cha Habari wa PPPC, Chelu Matuzya amesema maandalizi ya kongamano hilo yamekamilika na linatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya ubia katika maendeleo ya taifa.