Dar es Salaam. Tanzania imeondokewa na mmoja wa mashujaa wake, Dk Hassy Kitine, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) tangu 1978 hadi 1980.
Alikuwa pia mshauri wa karibu wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na mmoja wa viongozi waliokuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya usalama na ukombozi wa Afrika.
Dk Kitine ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81, aliwahi pia kuwa mbunge wa Makete na Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) anayesimamia Usalama wa Taifa.
Ibra Kitine, mtoto wa Dk Kitine amesimulia dakika za mwisho za baba yake aliyefariki dunia akiwa usingizini usiku wa kuamkia leo Julai 25, 2025 akiwa nyumbani kwake Oysterbay, Mtaa wa Laiboni 24, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, Ibra amesema baba yao baada ya kumaliza kula usiku wa jana Julai 24 alikwenda kulala na ndipo alipofikwa na mauti.
“Amefariki wakati amelala, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha yake,” amesema na kuongeza kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa miaka 40, ingawa kwa miaka mitatu iliyopita alipata pia maradhi ya utu uzima.
Akizungumzia taratibu za mazishi, Ibra amesema mwili wa baba yao utazikwa kesho Julai 26 baada ya sala ya saa 10:00 jioni kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
“Asubuhi utaletwa nyumbani hapa Oysterbay, kutoka Hospitali ya Jeshi Lugalo ulikohifadhiwa. Kutakuwa na ratiba nyingine hapa, baada ya sala ya saa 10:00 jioni, baba yetu atazikwa kwenye makaburi ya Kisutu,” amesema.
Amesema baada ya kustaafu, baba yao alipenda kukaa na wajukuu na alikuwa mfuatiliaji wa masuala ya siasa.
Alipenda watoto wake wasome na waishi vizuri na watu, kuwa na heshima, kuipenda nchi na kuheshimu maoni ya raia wengine.
Amesema baba yao alipenda kusema ‘tutafika’ kila alipozungumza nao.
“Ndilo neno ambalo lazima amalize nalo kuzungumza. Hata tukiwa tunakula, katika mazungumzo ya hapa na pale atahitimisha ‘tutafika’ akimaanisha hakuna ambacho kitashindika,” amesema.
Dk Kitine alizaliwa mwaka 1943 katika Kijiji cha Kisinga (sasa kinaitwa Ugabwa), Kata ya Lupalilo, Tarafa ya Lupalilo, Wilaya ya Makete.
Jina lake ‘Hassy’ si kifupi cha ‘Hassan’ kama ambavyo wengi wamekuwa wakifikiri, bali ni jina la asili la Kikinga alilotunukiwa na bibi yake.
Wakati wa utoto wake, familia ilipata msiba mkubwa alipofiwa na baba yake mwaka 1948, jambo lililomfanya ahamie Tukuyu mkoani Mbeya kwa shangazi yake akiwa na umri wa miaka minne.
Elimu ilikuwa msingi muhimu wa maisha ya Kitine. Alianza Shule ya Msingi Rungwe, Tukuyu mwaka 1950, baadaye akafaulu kwenda Shule ya Kati ya Ndembela mwaka 1954. Ubunifu wake wa kielimu ulionekana mapema alipomaliza Sekondari Malangali mwaka 1961, siku za Uhuru wa Tanganyika.
Mafanikio yake yakaendelea alipokwenda Shule ya Tabora Boys kwa masomo ya juu (darasa la 13 na 14) kabla ya kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1964 kusoma Shahada ya Uchumi.
Hapa ndipo alijumuika na wenzake kama Samuel Sitta (Spika wa zamani wa Bunge la Tanzania).
Wakati wa masomo yao walipata changamoto walipofukuzwa chuo kwa mwaka mmoja kutokana na maandamano, jambo lililowafanya wapoteze miaka miwili ya masomo, kwani walirejea shuleni mwaka 1968 badala ya 1967. Hata hivyo, bidii yao iliwafanya warejee na kumaliza masomo yao mwaka 1968.
Baada ya kuhitimu chuo kikuu, Dk Kitine alianza kazi ya ualimu katika Sekondari ya Ihungo, mkoani Kagera akifundisha uchumi kwa muda mfupi. Lakini, hatima yake ilikuwa imeandikwa mahali pengine. Mwaka 1969 alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Ruvu kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na kiwango chake cha juu cha elimu, alitambulika haraka na kupewa nafasi za uongozi. Baada ya miezi 18 katika JKT, alikuwa miongoni mwa vijana 10 walioteuliwa kubaki jeshini.
Marafiki zake kutoka shule za juu kama Godfrey Mang’enya na Peter Ligate walimhamasisha ahamie JWTZ (Jeshi la Wananchi wa Tanzania), ambako alipata mafunzo ya uofisa.
Mwaka 1971, akiwa Luteni mdogo, alipelekwa Uingereza kwa mafunzo ya uofisa kwa mwaka mmoja.
Aliporudi, aliteuliwa kuwa kamanda wa platuni Nachingwea, ambako alifanya kazi muhimu ya usalama wa mpaka na kusaidia harakati za ukombozi za Chama cha Freelimo cha Msumbiji dhidi ya wakoloni wa Ureno.
Kazi hiyo ilionyesha dalili za ubingwa wake wa kijeshi na uongozi. Mwaka 1971, aliteuliwa kuwa msaidizi wa mafunzo katika kuanzisha Chuo cha Maofisa cha Monduli (OCS), mahali ambako alibobea kama mwalimu wa siasa za kijeshi na mipango ya mafunzo.
Umahiri wake ulimfanya aongeze vyeo haraka, kutoka Luteni hadi Kapteni na hatimaye cheo cha Meja.
Mwaka 1976, wakati akiwa na umri wa miaka 33 tu, Dk Kitine alipokea wito ambao ulibadilisha maisha yake. Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania, alimteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) akiwa mmoja wa viongozi wachanga zaidi kushika nafasi hiyo muhimu nchini.
Mwalimu Nyerere alimjua Dk Kitine kwa muda mrefu kutokana na kazi yake katika Chuo cha Monduli, ambako Rais alikuwa akifika chuoni hapo kila mwaka kukamisheni maofisa wapya.
Kipindi chake katika TISS kilijiri wakati wa mabadiliko ya kiusalama na kisiasa, si tu nchini Tanzania bali Afrika nzima. Miaka ya 1970 na 1980 ilikuwa ni enzi za mapinduzi ya kijeshi katika nchi nyingi za Afrika na Tanzania ilihitaji uongozi makini wa usalama ili kulinda utulivu wa ndani, huku ikisaidia Bara la Afrika kujikomboa.
Dk Kitine alimrithi Dk Lawrence Gama na baada yake walikuja wakuu wengine kama Augustine Mahiga na Imran Kombe.
Uhusiano wa karibu kati ya Dk Kitine na Mwalimu Nyerere haukuwa rasmi tu, bali wa kina na wa kuaminiana.
Mwaka 1995 siku chache kabla ya uteuzi wa mgombea urais kupitia CCM, tukio muhimu lilitokea katika historia ya Tanzania.
Dk Kitine alimwendea Mwalimu Nyerere nyumbani kwake Msasani na kumweleza kuwa hakuna mgombea aliyestahili kutokana na migawanyiko ya makundi ndani ya chama. Inadaiwa alipoombwa amtaje mtu anayemuona anabebeka, Dk Kitine alimtaja Benjamin Mkapa, aliyekuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wakati huo.
Dk Kitine aliona kuwa Mkapa hakuwa na migawanyiko ya kikundi na alikuwa na historia safi, tofauti na wagombea wengine. Mwalimu Nyerere alikubali haraka na kumtuma Dk Kitine amuite Mkapa, ambaye baadaye alipata uteuzi wa CCM na kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hii ni moja ya mifano mikuu ya jinsi Dk Kitine alivyokuwa mshauri wa busara na mwenye uwezo wa kuona mbali katika masuala ya kisiasa ya nchi.
Nyadhifa serikalini, changamoto
Baada ya Mkapa kuchaguliwa, Dk Kitine aliingia kwenye siasa za uchaguzi na kuwa mbunge wa Makete baada ya kifo cha Tuntemeke Sanga. Pia aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na baadaye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayesimamia Usalama wa Taifa, nafasi muhimu katika ulinzi na usalama wa nchi.
Hata hivyo, maisha ya Dk Kitine hayakuwa bila changamoto. Mwishoni mwa miaka ya 1990, alihusishwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali kiasi cha Sh60 milioni, zilizodaiwa kuwa kwa ajili ya matibabu ya mkewe nchini Canada.
Tukio hilo liliibua mjadala na kumlazimu kujiuzulu. Hata hivyo, Dk Kitine daima aliamini kashfa hiyo ilikuwa njama ya kisiasa kuzuia azma yake ya kugombea urais. Alijibu madai hayo kwa uwazi, akieleza hakuna fedha za umma zilizotumika kwa makusudi yake binafsi.
Azma ya urais, maono ya kisiasa
Mwaka 2015, Dk Kitine alitangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM, akiahidi kurudisha maadili ya enzi za Mwalimu Nyerere.
Alisema: “Nipe miaka mitano tu, nitairejesha Tanzania ya Mwalimu.”
Alionya kuwa Ikulu si mahali pa kuficha udhaifu wala si biashara, bali ni uwanja wa wajibu na sadaka ya uongozi. Alisisitiza sifa muhimu kwa kiongozi ni uadilifu, uzalendo na heshima kwa Katiba.
Maono yake yalikuwa ya kurudi kwenye misingi ya utawala wa kwanza wa Tanzania, wakati wa uongozi wa busara na mazingira ya maadili.