Dar es Salaam. Katika kuhakikisha kuwa mkondo wa amali unazaa matunda kwa vijana waliopitia mfumo huo mpya wa elimu, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa wito kwa halmashauri zote nchini kuandaa mpango kazi wa kuwaweka pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zitakazozalishwa na wahitimu wa mafunzo hayo.
Wito huo umetolewa leo Julai 25, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Hussein Omar, alipotembelea Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa ajili ya kujifunza shughuli zinazotekelezwa na taasisi hiyo, hususan katika sekta ya elimu isiyo rasmi na mafunzo ya amali.
Mabadiliko hayo yalikuja kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa siku chache baada ya kuingia madarakani, akiitaka wizara hiyo kupitia upya mfumo wa elimu ili utoe wahitimu wenye ujuzi.
Hali hiyo ilisababisha kufanyika kwa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kupatikana toleo jipya la mwaka 2023 lililoweka msingi wa kuanzishwa kwa mkondo wa amali kuanzia kidato cha kwanza.
Kupitia mkondo huo, wanafunzi wanapata mafunzo ya fani mbalimbali ikiwemo ushonaji, useremala, biashara, uhandisi ujenzi, kilimo, ufugaji, usindikaji wa vyakula, uhandisi wa umeme, uchapishaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini, sanaa na ubunifu, pamoja na michezo.

Dk Omar amesema mkondo wa amali umeanzishwa kwa lengo la kuwapa vijana ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, lakini mafanikio ya mkondo huo hayawezi kupatikana kama hakutakuwepo na mazingira wezeshi ya kutumia ujuzi waliopata, ikiwemo upatikanaji wa masoko ya bidhaa zao.
“Tunataka vijana wasome wajiajiri lakini hilo haliwezekani kama hakuna soko, ndiyo maana nasema kuna haja ya wadau kujiandaa nikiweka msisitizo zaidi kwa halmashauri kwa sababu zenyewe ndiyo zina hawa vijana basi zianzishe vikundi kazi kulingana na utaalamu unaotolewa na ziwe tayari kutoa soko kwa bidhaa zitakazozalishwa.
“Mfano kwenye halmashauri ikaanzishwa kikundi cha ushonaji ikawasaidia vifaa hao vijana na kuwapa kazi inaweza kuwa kushona sare za wanafunzi wa halmashauri nzima. Hapo vijana watakuwa wamepata ajira na itaonekana tija ya hayo mafunzo ya amali na hata kuleta hamasa kwa wengine,”
Katika hatua nyingine, Dk Omar ameitaka TEWW kuweka mkakati madhubuti wa kuwabaini Watanzania wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), kwa kushirikiana na ofisi za mitaa, vijiji na vituo vya kutolea huduma, ili taifa liweze kuondokana kabisa na tatizo la ujinga.
Amesema, “Nimekutana na vijana wengi hawajui kusoma wala kuandika, natamani taasisi yenu ije na mkakati wa kuwabaini watu wa aina hii na hili linawezekana mkihusisha ofisi za mitaa na vijiji au hata maeneo ya kutolea huduma kama vituo vya afya.
“Licha ya jitihada zinazoendelea kufanyika kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kusoma anakwenda shule, bado kuna jamii hazina mwamko wa elimu na watoto hawasomi huko kote mnatakiwa muwafikie, mnaweza kuanza kwa kutoa mafunzo kulingana na shughuli wanazofanya kwenye jamii husika halafu mkaingizia KKK,”
Akizungumzia hilo Mkuu wa TEWW, Profesa Philipo Sanga amesema kulingana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 asilimia 17 ya watanzania hawajui kusoma na kuandika na taasisi hiyo imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha inapunguza idadi hiyo.
“Baada ya matokeo hayo, wizara ya elimu kupitia taasisi yetu kumekuwa na kampeni mbalimbali za kisomo na hivi karibuni tutazindua kampeni kubwa ya kitaifa ya kisomo inayolenga kuinua kiwango cha kisomo hapa nchini,” amesema Profesa Sanga.