Hijra ya Mtume tukio muhimu la Uislam-2

Makala iliyopita iliangazia historia kabla ya Hijra, mkakati wa Hijra, sababu za Mtume kuhama kutoka Makka kwenda Madina, matokeo ya kisiasa na ya kijamii katika Hijra, na tathmini ya wasomi wa kimagharibi kuhusu Hijra. Makala hii ni mwendelezo wa makala iliyopita… sasa endelea.

Hijra ya Mtume (S.A.W) haikuwa tu kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine, bali ilikuwa ni hatua ya kuanzisha jamii mpya inayojengwa juu ya maadili ya Kiislamu. Kupitia Hijra, Mtume wa Allah aliasisi dola inayojengwa juu ya misingi ya haki, usawa, utawala wa sheria na maadili mema.

Mtume wa Allah aliweka Mkataba wa Madina uliokuwa ni katiba ya kiraia. Mkataba huu uliweka utaratibu wa mahusiano kati ya wakazi wote wa Madina bila kujali tofauti za dini zao. Aliweka pia masharti ya mahusiano na makabila ya Kiyahudi yaliyokuwa yakiishi kandokando mwa mji wa Madina. Hii ilikuwa ni mfano bora wa kuvumiliana na kuishi kwa amani kati ya dini tofauti.

Kupitia Hijra, Mtume wa Allah aliunda dola ya Kiislamu iliyounganisha mamlaka ya dini na siasa. Hili lilichangia utulivu wa jamii, maendeleo ya kijamii, na kuonekana kwa sura kamili ya dola ya Kiislamu, ambapo Mtume wa Allah alikuwa ndiye kiongozi wa kisiasa, kijeshi, na pia mjumbe wa Allah.

Baada ya Hijra, Waislamu walipata jeshi lililoandaliwa vizuri. Hii iliwapa uwezo wa kujilinda dhidi ya watesaji wao waliowafuata, na pia kueneza uislamu katika maeneo mbalimbali duniani kwa njia ya hekima, ulinganizi na uadilifu.

Athari za kiuchumi za Hijra

Hijra ya Mtume (S.A.W) haikuwa tu mabadiliko ya kijamii na kisiasa, bali pia ilikuwa na athari kubwa za kiuchumi kwa jamii ya watu wa Madina, ambayo awali ilitegemea kilimo na biashara.

Kuwasili kwa Waislamu wahamiaji (Muhajirina), mji wa Madina ulianza kushuhudia ongezeko la shughuli za kiuchumi. Muhajirina walileta pamoja nao ujuzi mbalimbali, mtandao wa biashara kutoka Makka na maeneo ya mbali, jambo lililosaidia kukuza uchumi wa mji huo na kuleta ustawi katika jamii mpya ya Kiislamu.

Hijra ilikuwa na athari nyingi za kiutamaduni na kielimu. Madina ikawa kitovu cha elimu na maarifa. Waislamu walijifunza kutoka kwa tajiriba zao za awali huko Makka, na pia walinufaika na tamaduni za watu waliowazunguka.

Mtume wa Allah aliandaa darasa na semina (halqa) za elimu, akiwafundisha Waislamu mambo ya dini yao na masuala ya maisha ya kila siku. Hatua hizi zilisababisha mwamko mkubwa wa kielimu na kitamaduni, na hivyo kuweka msingi wa maendeleo ya maarifa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Changamoto zilizokabili Hijra

Licha ya mafanikio makubwa ya Hijra, tukio hili halikukosa changamoto na matatizo. Mtume Muhammad wa Allah na Maswahaba wake walikabiliwa na vizingiti vingi, vikiwemo vitisho vya ndani kutoka kwa wanafiki na baadhi ya makabila ya Kiyahudi waliokuwa wakipinga ujenzi wa dola mpya.

Kulikuwepo pia na vitisho vya nje kutoka kwa washirikina wa Kikuraishi waliotumia mbinu za kijeshi na kisiasa ili kuangamiza dola changa ya Kiislamu. Changamoto za kiuchumi na kijamii zilihitaji suluhisho la haraka ili kujenga jamii imara na yenye mshikamano.

Changamoto hizi zote zilihitaji busara, subira, na uongozi thabiti kutoka kwa Mtume wa Allah na Maswahaba zake.

Hijra ya Mtume wa Allah ni tukio muhimu katika historia ya Uislamu na ulimwengu kwa ujumla. Kama tafiti za kisasa na maoni ya wanazuoni wa kimagharibi zinavyobainisha, Hijra haikuwa tu safari ya kimazingira kutoka Makka kwenda Madina, bali ilikuwa ni hatua ya kistratejia iliyosababisha:

Kuasisiwa kwa dola ya Kiislamu, kusimikwa kwa nguvu ya Uislamu katika Rasi ya Uarabuni (Jaziratul Arab), kKuenea kwa mafundisho ya Kiislamu duniani kote baadaye.

Uchambuzi wa kina wa tukio hili unatuwezesha kufahamu vyema historia ya Uislamu na jinsi jamii za Kiislamu zilivyopitia hatua mbalimbali za maendeleo katika nyakati tofauti.

Hijra inatufundisha kuwa kwa nia madhubuti na uongozi wenye hekima, haiwezekani huwa jambo la kufikirika tu, bali linaweza kuwa jambo halisi. Changamoto kubwa zinaweza kugeuzwa kuwa fursa za kuunda maisha bora zaidi katika nyanja zote.

Ujumbe huu wa Hijra unaendelea kuwa na maana hadi leo, na unaweza kutumika kama rejea ya kujenga jamii za kisasa zilizojaa amani, mshikamano na maendeleo endelevu.