Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imepanga Agosti 22, 2025 kutoa hukumu kesi ya mauaji ya mwanafamilia inayomkabili Sophia Mwenda (64) na mwanaye wa kiume Alohonce Magombola (39).
Sophia na mwanawe wanadaiwa kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti yake wa kwanza wa kumzaa mwenyewe kwa kumchoma kisu chini ya titi, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba mosi, 2020 Kijichi, Wilaya ya Kigamboni.
Uamuzi huo umetolewa leo, Julai 25, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, aliyeongezewa mamlaka ya ziada kusikiliza kesi ya mauaji.
Hakimu Mrio amepanga tarehe hiyo, baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao wa mashahidi wanne wakiwemo watuhumiwa wenyewe.
“Baada ya washtakiwa kumaliza kujitetea pamoja na mashahidi wa upande wa utetezi, Mahakama hii inapanga Agosti 22, mwaka huu kutoa hukumu katika kesi hii,” alisema Hakimu Mrio na kuongeza
“Hivyo, mawakili wa pande zote mbili mnatakiwa kuwasilisha majumuisho yenu kwa njia ya maandishi Agosti 4, 2025,” alisema hakimu
Julai 11, 2025 Mahakama hiyo iliwakuta na kesi ya kesi ya kujibu washtakiwa hao, upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.
Upande wa mashtaka uliita mashahidi 22 na vielelezo tisa ambao walitoa ushahidi wao mahakamani hapo kuhusiana na kesi hiyo ya mauaji.
Hata hivyo mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Hilda Mushi na Godwin Fissoo, waliieleza mahakama hiyo wanatarajia kuwa na mashahidi wanne kila mmoja wakiwemo washtakiwa hao pamoja na vielelezo.
Katika utetezi wake, mshtakiwa kwa kwanza katika kesi hiyo, Alphonce alidai kuwa hahusiki na kifo cha dada yake.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa utetezi Hilda Mushi, Alphonce alidai kuwa hajawahi kupelekwa Bagamoyo kwenda kuonyesha askari Polisi sehemu ambayo mwili wa Beatrice ulitupwa na kama ingekuwa ni kweli basi hata mwenyekiti wa eneo hilo au askari polisi wa Bagamoyo wangekuja kutoa ushahidi wao.
Pia, hajawahi kupelekwa Kijichi kwenda kuchora ramani ya tukio la mauaji kama mashahidi wa upande wa mashtaka walivyodai.
Katika ushahidi aliyotoa Sophia alidai kuwa yeye ni mfanyabiashara wa mazao na makazi yake ya kudumu ni Moshi mkoani Kilimanjaro na Mbeya.
Pia, amedai kuwa hauhusiki na kifo cha mwanae kwa sababu taarifa za kifo hicho yeye alikuwa Moshi.
Pia, alikamatwa Machi 17,2022 wakati akiwa hospitali ya Zakhiem akiwa katika foleni ya kumuona daktari, hivyo hausiki na kifo cha Beatrice.
“Niliajiriwa serikalini huko mkoani Morogoro na mume wangu aliajiriwa Serikali za mitaa na mwaka 1986 tulifunga ndoa na kubahatika kupata watoto wanne,” alidai Sophia.
“Mwaka 1994, mume wangu alioa mke mwingine huko Mbeya na mimi sikufurahia jambo hilo, hivyo nilienda kwa Askofu kulalamika,” alidai.
Aliendelea kujitetea kuwa mwaka 1995 alinunua kiwanja mkoani Mbeya na mwaka 1996 alianza ujenzi na mwaka 1998 na baada ya hapo alienda nchini Uganda kusoma.
Shahidi huyo alidai pia alipigwa na kuteswa wakati akiandika maelezo ya onyo polisi na kupelekea kuumia jicho lake.
Baada ya kutoa utetezi wake, Sophia aliulizwa maswali ya dodoso na wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema na sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo.
Wakili: Shahidi una nyaraka au kielelezo chochote ulichokiwasilisha mahakamani hapa kuonyesha kuwa ulipata ulipata matibabu katika hospitali ya Magereza?
Wakili: Kwanini hukumhoji shahidi wa upande wa mashtaka aitwaye Nicolas, ambaye ulidai kuwa alikutesa na kukupiga kibao usoni upande wa kushoto na kichwani alipofika mahakamani hukumhoji
Wakili: Wewe na aliyekuwa mume wako, mlikuwa na mgogoro wa nyumba Mbeya?
Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa aliyekuwa mume wako, alieleza Mahakama kuwa kulikuwa na shauri la mgogoro namba 134/ 2020 huko Mbeya?
Shahidi: Ni sahihi alieleza
Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba mahakama hii ina uwezo wa kupata kumbukumbu ya shauri la mgogoro ambalo lilikuwepo Mahakamani Mbeya? Shahidi: Mahakama ina uwezo.
Wakili: Unafahafamu madhara ya kusema uongo katika Mahakama hii ukiwa chini ya kiapo?
Shahidi wa nne wa upande wa utetezi, Rachel Magombola(35) ambaye ni mtoto wa tatu wa Sophia alidai kuwa yeye alipewa taarifa za kifo cha Beatrice akiwa Zanzibar.
Rachel ambaye anaishi Zanzibar eneo la Fuoni Mambosasa na anafanya kazi ya kuwatembeza watalii, alidai kuwa mpaka sasa hawezi kujua alipo na mara ya mwisho kuongea na Beatrice ilikuwa kati ya Oktoba hadi Novemba mwaka 2020.
“Tuliongea naye mambo ya kifamilia na kipindi hicho kulikuwa na korona hivyo niliyumba kibiashara , hivyo tulikuwa tunajadiliana namna ya kusaidia” alidai Dada yangu alikuwa ni mtu wa kujifanyia mambo yake bila ndugu zake kujua na kuna wakati hakutaka kushirikisha ndugu zake katika mambo yake.
Alidai yeye na marehemu Beatrice hawakuwa na mawasiliano ya karibu, kama ilivyo kwa Alphonce na Desdeus, ambapo huwasiliana mara kwa mara.