Mbeya. Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka wasimamizi, waratibu na maofisa wa uchaguzi kuhakikisha wanasimamia mabango, matangazo na orodha ya majina kutoka tume yanabandikwa sehemu sahihi na kwa wakati ili kuepuka malalamiko ya ukiukwaji wa masharti ya sheria na kanuni za uchaguzi.
Pia imewataka kutunza siri na kutotoa taarifa kwenye vyombo vya habari zenye kuleta taharuki na badala yake kabla ya kufanya hivyo, wajiridhishe na usahihi au kushirikisha watalaamu na kujiweka mbali na makundi sogozi kutotuma taarifa ambazo hazikupaswa kwenda huko.
Hayo yameelezwa Julai 23 na Ofisa mwandamizi Tume ya huru ya Tume ya Taifa, Daniel Kalinga wakati wa kufunga mafunzo ya waratibu wa uchaguzi Mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi ngazi ya jimbo, maafisa uchaguzi na maofisa ununuzi kutoka Mikoa ya Mbeya na Songwe.
Amesema changamoto zilizojitokeza wakati wa uboresho ya daftari la kudumu la mpiga kura za kutobandika mabango maeneo husika ili kumuelekeza mwenye sifa kujiandikisha na wadau wengine kujua mahali kilipo kituo na kuwataka kutojirudia kipindi hiki cha uchaguzi.
Amewataka washiriki hao wa mafunzo kuhakikisha wanajiridhisha orodha waliyonayo kutoka Tume, taasisi yoyote inayotoa elimu ya utoaji elimu ya mpiga kura, vinginevyo wawasilishe haraka taarifa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi.
“Moja ya majukumu wenu ni kupokea na kukagua vitambulisho na barua za watendaji wa asasi na taasisi zilizopewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura au kuwa waangalizi wa uchaguzi, hakikisha mnajiridhisha katika orodha uliyonayo wamepangiwa jimbo lako,” amesema.
“Usije kupokea watu ambao hawajatumwa na Tume na iwapo utabaini hivyo, toeni taarifa haraka na mapema kwa ajili ya hatua zaidi, hakikisha asasi na taasisi hizo zinatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria” amesema Kalinga.
Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Gidion Mapunda amesema mafunzo hayo yamejikita katika maeneo mbalimbali ikiwamo maadili ya kampeni, maadili ya upigaji kura na utoaji matokeo, utunzaji vifaa vya uchaguzi, kura za Rais na sheria za gharama za uchaguzi.
Amesema siku tatu walizotumia kwenye mafunzo hayo, yamewajenga vyema na wako tayari kwa ajili ya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo yote ya uchaguzi.
“Tumekuwa na mafunzo mazuri ambayo yametujenga vyema, tumepitia mada mbalimbali kuhusu uchaguzi kama wateuzi wa wagombea, wajibu wa watendaji katika vituo na usimamizi wa fedha,” amesema Mapunda.