KOCHA mkongwe anayeshikilia rekodi ya kuwa kocha mzawa aliyebeba mataji kwa misimu miwili mfululizo, John Simkoko amesema tayari Mtibwa Sugar itakuwa imepata funzo kujua kipi kiliishusha msimu wa 2023/24 na anatarajia kuona itarejea msimu ujao kwa nguvu kubwa na ushindani wa ligi.
Simkoko aliyewahi kuifundisha timu hiyo miaka ya nyuma, ndiye aliyeipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara misimu ya 1999 na 2000 na aliliambia Mwanaspoti, Wakata Miwa hao wanatakiwa kusajili kikosi imara, kujenga umoja kuanzia kwa viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki na kuanza maandalizi ya mapema yatakayoendana na ushindani wa ligi ijayo.
“Ligi ya msimu ujao itakuwa ngumu, nafuatilia usajili unaofanywa na timu, makocha wa kigeni wanaokuja Tanzania, hilo linatoa picha ya ushindani mkali, ndiyo maana nasisitiza lazima Mtibwa ijipange kisawasawa na jambo la msingi zaidi ni kuhakikisha inashinda mechi za mwanzo ili za mwishoni ziwe za mahesabu za nafasi za juu siyo kujikwamua na kushuka daraja,” alisema Simkoko ambaye kwa sasa ni Meneja wa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Alisema uwepo wa wachezaji wa kigeni unaongeza thamani ya Ligi Kuu, pia inawapa chalenji wazawa kupambana kuhakikisha viwango vyao vinakuwa juu kwa faida ya timu zao na Taifa Stars.
“Zamani wachezaji wazawa walikuwa wanatoka kwenda kucheza nje, ila kwa sasa wageni ni wengi katika ligi yetu, ndiyo maana naishauri Mtibwa ijipange ili iwe mfano wa kuonyesha vipaji na viwango vya wazawa kuwa juu,” alisema kocha huyo.
Simkoko aliiongoza Mtibwa kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara mwaka 1999 na 2000 katika kikosi chake kulikuwepo wachezaji kama Mecky Maxime, Kassim Mwabuda, Kassim Issa, Monja Liseki, Zubery Katwila, Godfrey Kikumbizi, Abdallah Juma, Salhina Mjengwa na Abubakar Mkangwa.
“Ninachojivunia ni kuwaona wachezaji ambao niliwafundisha wengi wao ni makocha katika timu mbalimbali na wanafanya kazi nzuri,” alisema.