TAASISI ya Kilombero Community Charitable Trust (KCCT), kwa kushirikiana na Kampuni ya Kilombero Sugar Company Limited (KSCL), imefanikiwa kutoa mafunzo na kuwatunuku vyeti wakulima 734 wa miwa kutoka vyama 17 vya ushirika (AMCOS) kupitia mpango wa Elimu Tija katika Bonde la Kilombero.
Mpango huu wenye mwelekeo wa kubadilisha maisha ya wakulima ulikuwa na mafunzo ya kina yaliyolenga kuongeza tija katika uzalishaji, kuwawezesha kifedha, kukuza uelewa wa utunzaji wa mazingira na kuwapa mbinu bora na za kisasa za kilimo cha miwa. Wakulima wote walikamilisha moduli tano za mafunzo na kutunukiwa vyeti kama uthibitisho wa juhudi na mafanikio yao.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo,Julai 24, 2025 mkoani Morogoro, Mgeni Rasmi ambaye alimwakilisha, Bi. Pilly Kitwana , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara. alisema:
“Nawapongeza KCCT na Kilombero Sugar kwa uwekezaji wao mkubwa katika elimu ya wakulima. Mafunzo haya ni zaidi ya maarifa; yanatoa msingi imara wa mabadiliko ya kweli katika maisha ya wananchi wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote kuendeleza jitihada hizi muhimu kwa maendeleo ya jamii ya Kilombero.”
Kwa upande wake, Bw. Guy Williams, Mkurugenzi Mtendaji wa Kilombero Sugar na mdhamini mkuu wa mpango huu, alisema:
“KCCT imekuwa mstari wa mbele kwa zaidi ya miaka 25, na Kilombero Sugar imeendelea kuwa mshirika mkuu katika kusaidia juhudi hizi. Nawapongeza wakulima wote waliokamilisha mafunzo haya na nawahimiza kutumia maarifa waliyoyapata ili kuboresha kilimo chao na maisha yao kwa ujumla.”
Mwenyekiti wa Bodi ya KCCT, Bw. Derick Stanley, alieleza kuwa uhitaji wa elimu kwa wakulima unazidi kuongezeka:
“Kwa zaidi ya miaka 25, KCCT imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali, huku Kilombero Sugar ikiwa mshirika wa muda mrefu. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuungana nasi katika kuwawezesha wananchi wa Kilombero. Kupitia mradi wa upanuzi wa K4 unaotarajiwa kuanza, wakulima wanayo nafasi ya kipekee kutumia maarifa haya ili kufaidika na ongezeko la mahitaji ya miwa.”
Naye Bw. Pierre Redinger, Mkurugenzi wa Wakuzaji Miwa wa Kilombero Sugar, alisema: “Kuwawezesha wakulima kwa ujuzi wa vitendo ndiyo njia bora zaidi ya kuleta mabadiliko ya kudumu katika sekta ya kilimo. Tumeshuhudia mwitikio mkubwa na hamasa ya kujifunza kutoka kwa wakulima. Sasa tunatarajia kuona ongezeko la tija na maendeleo ya kina katika kilimo cha miwa.”
Bi. Willa Haonga, Kaimu Meneja wa KCCT, alifafanua kuwa mafunzo haya yalitolewa kwa kutumia moduli tano zilizoratibiwa vizuri, kwa kushirikiana na wadau waliotoa msaada katika elimu ya mazingira, uelewa wa masuala ya fedha na ujasiriamali.
Wakulima walionufaika na mpango huu walitoa shukrani zao na kuomba mafunzo haya yaendelezwe zaidi. Walisema kuwe na mashamba darasa na vifaa vya kujifunzia ili kuongeza uelewa wa vitendo na kuboresha zaidi kilimo chao.