Monduli. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi ameonya wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali wilayani Monduli kutokuwa wazembe na kuwa kusiwepo miradi ‘kichefuchefu’ wilayani humo.
Amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuheshimu vyombo vya ulinzi na usalama kwani vina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na wamekuwa wakijitoa kuhakikisha Taifa linakuwa salama.
Kihongosi ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 25, 2025 kwenye ziara yake wilayani Monduli akikagua miradi ya maendeleo ambapo amekagua mradi wa maji katika Kijiji cha Esilalei na ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Manyara.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi huo wa bweni litakalogharimu zaidi ya Sh174.7 milioni, Kihongosi ameagiza miradi yote inayotekelezwa wilayani humo isiwe “kichefuchefu”.
“Nipongeze utekelezaji wa mradi huu unaridhisha hivyo niagize wilayani humu miradi kichefuchefu isiwepo Monduli, tekelezeni miradi yenye ubora,” amesema.
Kuhusu maadili, Kihongosi amesema kwa sasa maadili yameharibika na kumekuwa na vitendo visivyo vya kimaadili ikiwemo ubakaji na ulawiti na kuwataka wazazi na walezi kushirikiana na walimu kusimamia malezi.
Mkuu huyo wa mkoa amemwagiza Ofisa Elimu Sekondari wilayani humo kutokuwasumbua walimu akiwemo mkuu wa shule hiyo, Kimbele Njake.
“Kazi ya hapa ya ujenzi wa mabweni itadumu, walimu mliopo hapa mkiongozwa na Mkuu wa Shule, msiwasumbue walimu kama hawa, kuna uhamisho unatokea ghafla, kwa huyu labda mumpandishe cheo, msimpeleke shule ndogo, mwacheni achape kazi,” amesema.
Akisoma taarifa za ujenzi wa shule hiyo, Mtendaji wa Kijiji cha Losirwa, Natuli Leiyo amesema shule hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1991, ina wanafunzi 1,493, kati yao 125 ni wenye mahitaji maalumu.
Amesema ujenzi wa bweni hilo lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 120 hadi kukamilika kwake, utagharimu Sh174.7 milioni unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wanaochangia Sh154.7 milioni huku nguvu kazi ya wananchi ikiwa Sh20 milioni.
“Hadi sasa mradi umegharimu Sh138 milioni na tunatarajia utakamilika Agosti 15, 2025 na utasaidia wanafunzi kupata mazingira mazuri kwa ajili ya malazi hapa shuleni,” amesema.
Mmoja wa wanafunzi hao, anayesoma kidato cha tatu, Glory Daniel amesema ujenzi wa bweni hilo jipya utaongeza mazingira salama kwa wanafunzi wa kike.
“Ujenzi wa bweni hili utasaidia wanafunzi wa kike kuepuka vishawishi wanavyokutana navyo barabarani na kuweza kufikia ndoto zetu,tutapata muda wa kujisomea zaidi kwani hatutakuwa tukitembea umbali mrefu kuja shuleni,” amesema.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Kimath ametaja moja ya changamoto kubwa wilayani humo ni migogoro ya ardhi ambayo inachangiwa na uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi juu ya sheria na tafsiri ya mipaka.
“Wilaya yetu ina changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo inasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo utawala na uongozi, uelewa mdogo wa wananchi wetu juu ya sheria ya ardhi na kutafsiri matumizi na mipaka,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Esilalei, Isaya Kayai amesema kipindi cha nyuma kabla ya kukamilika kwa mradi huo wa maji uliogharimu zaidi ya Sh1 bilioni wanawake walikuwa wakiteseka kufuata maji umbali mrefu.
“Kipindi cha nyuma, akina mama walikuwa wanateseka, wengine wanatembea hadi umbali wa kilomita 12 kufuata maji, walikuwa wanakumbana na wanyama wakali na changamoto nyingi lakini kwa sasa mradi huu unawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa sababu hawatumii muda mrefu tena kufuata maji,” amesema.