Maafande wa JKT Tanzania kumng’oa beki Yanga

MAAFANDE wa JKT Tanzania wapo siriazi na usajili wa beki kinda wa Yanga, Isack Mtengwa, ikielezwa wanajeshi hao wako katika mpango wa kuvunja mkataba ili kumnunua moja kwa moja.

Msimu uliopita, nyota huyo aliichezea Wakiso Giants ya Uganda kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Yanga U-20, akiungana na beki mwenzake Shaibu Mtita.

Akizungumza na Mwanaspoti, kiongozi mmoja wa JKT (jina tunalo) alisema tayari wamepeleka ofa ya kuvunja mkataba wa kinda huyo, hivyo wanasubiri majibu kutoka kwa Wananchi hao.

Aliongeza kama wataikataa ofa yao, basi wataangalia utaratibu wa kumchukua kwa mkopo hadi atakapomaliza mkataba wake.

“Tulizungumza naye lakini hatukujua kama alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja, hivyo ikabidi tuongee na timu yake. Tunasubiri tu majibu na kama tutashindwana tutaangalia, ila naamini tutafikia pazuri,” alisema kigogo huyo wa JK T na kuongeza:

“Kocha Ahmad Ally amemfuatilia na amesisitiza kuwa naye msimu ujao, hivyo tunapambana kuongeza damu changa eneo la pembeni kwa sababu kuna asilimia ya waliokuwepo kuondoka. Hivyo, Mtengwa anaweza kuwa mbadala wake,” kilisema chanzo hicho.