Dar es Salaam. Kuwa na kisukari haina maana kuwa huwezi kupata ujauzito salama.
Hata hivyo, ni muhimu sana kwa mwanamke mwenye kisukari kupanga ujauzito wake kwa umakini, kwa kushirikiana na wataalamu wa afya.
Hatua hii ya maandalizi husaidia kupunguza hatari kwa mama na mtoto, hasa katika hatua za mwanzo za ujauzito, ambapo viungo vya mtoto huanza kutengenezwa.
Kwa wanawake wenye kisukari, kuwa na viwango vya juu vya sukari kabla ya kushika ujauzito, huongeza hatari ya matatizo mbalimbali kama vile mtoto kuzaliwa kabla ya wakati, kuharibika kwa mimba, au mama kuwa na shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito. Kwa hiyo, kuwa na usimamizi mzuri wa viwango vya sukari kabla ya ujauzito, hupunguza sana hatari hizi. Kabla ya ujauzito, mwanamke wenye kisukari lazima azingatie yafuatayo
Mosi, viwango vya sukari, lengo likiwa kuhakikisha kuwa kiwango cha HbA1c ambacho ni kipimo cha wastani wa sukari kwa miezi 2–3, kiko ndani ya viwango salama. Inashauriwa iwe chini ya asilimia 6.5 kabla ya kushika mimba, ili kupunguza uwezekano wa mimba kuharibika na changamoto zingine.
Pili, Wasiliana na daktari mapema.Huduma ya kabla ya ujauzito inahusisha timu ya wataalamu, kwa maana ya daktari wa kisukari, daktari wa wanawake na mtaalamu wa lishe. Hawa wote husaidia kuhakikisha kuwa mwili wako uko tayari kwa ujauzito.
Tatu, kuzingatia matumizi ya dawa na lishe, baadhi ya dawa zinazotumika kudhibiti kisukari au shinikizo la damu hazifai kutumiwa wakati wa ujauzito. Daktari atakusaidia kubadilisha dawa.
Kuzingatia matumizi ya dawa za asidi ya foliki. Wanawake wanashauriwa kuanza kutumia folic acid angalau mwezi mmoja kabla ya kushika mimba ili kusaidia ukuaji wa neva kwa mtoto. Lishe sahihi si tu kwamba husaidia kudhibiti kisukari, bali pia hujenga mwili wa mama kuweza kuhimili ujauzito.
Mtaalamu wa lishe anaweza kusaidia kupanga mlo ambao unazingatia mahitaji ya kiafya ya mama na mtoto.
Nne, kujua hali ya macho, figo na moyo. Ni muhimu kujua afya ya viungo hivi kabla ya kupata ujauzito, hakikisha macho, figo, na moyo vimekaguliwa ili kuhakikisha vinaweza kuhimili ujauzito bila matatizo.
Tano, kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe, tabia hizi huongeza hatari kipindi cha ujauzito na huathiri ukuaji wa mtoto tumboni.
Wanawake wengi wanaoishi na kisukari wanaweza kupata ujauzito salama na kujifungua watoto wenye afya bora. Muhimu ni kuwa na maandalizi ya mapema, elimu sahihi, na kushirikiana na wataalamu wa afya.
Kuwa na kisukari hakikuzuii kuwa mama, ila unahitaji nidhamu ya lishe na matumizi ya dawa na kuhudhuria kliniki ya kisukari mara kwa mara.