Wakati zikibaki siku nane (8) kabla ya kuanza kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Morocco amewataka wachezaji wa Simba na Yanga kuwa chachu ya mafanikio ya timu hiyo kwenye fainali hizo.
Taifa Stars iliyo katika kundi B la mashindano hayo, imepewa fursa ya kucheza mechi ya ufunguzi wa fainali hizo ambayo itafanyika Jumamosi, Agosti 2, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Morocco ambaye amesema kuwa kufika hatua ya mtoano itakuwa ni mafanikio makubwa kwa timu yake, anaamini Taifa Stars inaweza kufanya makubwa ikiwa nyota wa Yanga na Simba katika kikosi chake watahamisha kile wanachokifanya klabuni kwenda katika timu ya taifa.
“Wachezaji kutoka klabu kama Simba na Yanga tayari wameonyesha wanaweza kushindana katika ngazi za juu za mashindano ya CAF.
“CHAN ni nafasi kwao kuthibitisha katika timu ya taifa. Kufika hatua ya mtoano itakuwa mafanikio makubwa lakini lakini kupata wachezaji watakaokuwa na nafasi ya mara kwa mara Taifa Stars ni jambo lenye thamani,” amesema Morocco.
Kocha huyo pia amefichua kwamba eneo linalompa matumaini zaidi katika kikosi chake ni safu ya ulinzi ingawa pia safu ya kiungo inatia matumaini.
“Naamini tuna kikosi kilicho na uwiano lakini mpangilio wetu wa ulinzi ni nguzo. Tuna safu ya ulinzi yenye uzoefu na ngumu ambayo inafahamu mahitaji ya mashindano makubwa.
“Katika kiungo kuna mchanganyiko mzuri wa nishati, maono na nidhamu unaoturuhusu kutawala mchezo. Safu ya ushambuliaji inaendelea kujenga muunganiko wake lakini tumeziona nyakati zinazotoa matumaini,” amesema Morocco.
Kocha huyo anaamini uwepo wa wachezaji baadhi wenye kariba ya uongozi utakuwa msaada mkubwa kwa kikosi kwenye CHAN.
“Uongozi katika kundi pia ni aseti kubwa. Baadhi ya wachezaji wanaleta ukomavu na weledi. Kimsingi mpira wa miguu unabadilika na uimara wa kwenye makaratasi unatakiwa kuthibitishwa uwanjani.
“Kiwango cha maandalizi kinatengeneza daraja na kinaashiria nia yetu nzito. Mafanikio yanaanza na upangaji mzuri na tunaamini tupo katika njia sahihi,” amesema Morocco.
Hii ni mara ya tatu kwa Taifa Stars kushiriki CHAN baada ya kufanya hivyo katika fainali za 2009 na 2020 ambapo mara zote iliishia katika hatua ya makundi.