Ruvuma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia mtuhumiwa Wende Luchagula (30), Mkazi wa Kijiji cha Milonji kwa tuhuma za mauaji ya watoto watatu wakiwamo pacha wawili ambao ni wa mke mdogo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya tukio hilo lilitokea Julai 12, 2025 saa nane mchana katika Kijiji cha Milonji, Kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo ambapo mtuhumiwa anadaiwa kutumia kitu chenye ncha kali kufanya mauaji hayo baada ya mume wake na mke mwenzie kwenda mnadani.
“Taarifa kamili ni kwamba, mume wa mtuhumiwa huyo alikuwa ameoa wake watatu lakini alikuwa akimpenda zaidi mke mdogo na watoto wake kitendo ambacho mtuhumiwa hakukipenda ndipo akavizia mume wake na mama mzazi wa watoto hao ambaye ni mke mdogo wakiwa wameenda mnadani kisha akatekeleza tukio hilo la kikatili. Miili ya marehemu tayari imekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi,”imeeleza taarifa hiyo ya Polisi.
Aidha, kupitia taarifa hiyo Jeshi la Polisi limetoa wito na kuwaasa wanandoa ambao wameridhia kuolewa kwenye ndoa ya zaidi ya mke mmoja kuhakikisha wanakuwa wavumilivu na kutokuwa na wivu wa kupindukia baina yao na pale inapotokea migogoro yoyote ndani ya ndoa zao nawashauri kutumia njia sahihi ya kutatua migogoro hiyo au kuwashirikisha viongozi wa dini au wazee mashuhuri kusaidia kutatua migogoro hiyo kwa amani.
“Jeshi la Polisi linaendelea kuhimiza jamii kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya amani na kuepuka vitendo vya ukatili ambavyo vinahatarisha maisha ya watu wasio na hatia, hasa watoto,”imeeleza taarifa hiyo.