Mbatia ataka mazungumzo ya kitaifa kuleta utulivu wa kisiasa

Dar es Salaam. Wakati akiwa kwenye mgogoro na chama chake licha ya kushinda kesi ya kuvuliwa uongozi na kufutwa uanachama, mwenyekiti wa zamani wa NCCR Mageuzi, James Mbatia amesema mustakabali wake kisiasa kwa sasa ni “Tanzania kwanza”.

Pia, amesema kuna haja ya kuwa na mazungumzo ya kitaifa yanayohusisha makundi mbalimbali ili kuondokana na hali ya sintofahamu inayoendelea sasa ya watu kutekwa, kupotezwa au kuuawa na watu wasiojulikana.

Mbatia amebainisha hayo leo Julai 25, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu hali ya kisiasa nchini, ambayo ameeleza kuwa ni mbaya na ikiachwa ikaendelea, itavuruga amani ya nchi.

Septemba 24, 2022, mwanasiasa huyo mkongwe aliondolewa madarakani na halmashauri kuu ya NCCR Mageuzi na kumvua uenyekiti, jambo ambalo lilimfanya Mbatia kufungua shauri mahakamani kupinga uamuzi huo wa halmashauri kuu.

Mahakama Kuu ya Tanzania imefuta uamuzi wa kumfuta uanachama na kumuondoa Mbatia katika nafasi ya uenyekiti wa taifa wa NCCR Mageuzi, ikisema uamuzi huo ulikuwa batili kisheria.

Uamuzi huo umetolewa Mei 28, 2025 na Jaji Abdi Kagomba wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wakati akitoa uamuzi katika maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review) aliyoyafungua dhidi ya bodi ya wadhamini ya chama hicho.

Katika uamuzi wake huo, Jaji Kagomba alisema uamuzi wowote ambao hauzingatii haki ya asili unapaswa kufutwa, hivyo mahakama inafuta uamuzi wa kumfuta uanachama na kumvua uongozi Mbatia, uliofikiwa Septemba 24, 2022.

Licha ya ushindi huo, Mbatia amekuwa kimya wakati wote tofauti na matarajio ya wengine ambao walitarajia kwamba angerejea madarakani mara moja kuendelea na uongozi katika chama hicho alichoshiriki kukiasisi.

Akizungumzia mustakabali wake katika siasa, Mbatia amesema kwa sasa anazingatia Taifa kwanza ili kuhakikisha kwamba hali ya kisiasa inakaa vizuri na kila Mtanzania afurahie kuwa Mtanzania, badala ya kuishi kwa hofu.

“Mimi kwa kipindi hiki nasema kweli Tanzania kwanza, na ndiyo maana nimekuwa na utulivu wa fikra, madhila yote haya yaliyotokea, sikuwahi kupiga kelele. Unajua ukikosa utulivu wa fikra, unakosa kuwa na maono mapana na kujifunza,” amesema.

Amesisitiza kwamba ni muhimu kusikiliza sauti za Watanzania kuhusu maisha yao kwani nchi hii ni yao na wana haki ya kuamua kuhusu maisha yao. Amesema maridhiano ndiyo njia pekee ya kutibu majeraha yanayolisibu taifa hili.

“Tusikilize Taifa letu linasema tufanye mazungumzo, tuje pamoja kabla ya kufanya jambo lolote, turidhiane. Hatutaki tumwage damu ya mtu, kwa sababu tukielewana vizuri, Tanzania itashinda, nafasi hiyo ipo.

“Ninaamini kabisa tukijisikiliza, tukasikilizana kila mmoja, tutatoka salama, lakini tukiendelea kama tunavyoendelea sasa hivi…hapatatosha. Tusichezee amani yetu, tusiruhusu machafuko, tunayo nafasi, tunao utamaduni,” amesema.

Mbatia amesisitiza kwamba ni muhimu kukumbatia hekima kwani ni moja ya nguzo muhimu zilizobainishwa kwenye Wimbo wa Taifa ambazo ni hekima, umoja na amani. Ameongeza kwamba hekima ni zaidi ya Katiba, sheria na kanuni katika utatuzi wa changamoto ambazo taifa linapitia.