Mghana aingia anga za Azam FC

MABOSI wa Azam FC wanafanya maboresho ya timu hiyo kwa ajili ya kuhakikisha msimu ujao wanaleta ushindani mkubwa, ambapo kwa sasa inadaiwa wameanza mazungumzo ya kuiwinda saini ya beki wa kushoto wa Singida Black Stars, Mghana Ibrahim Imoro.

Imoro aliyejiunga na timu hiyo Julai 1, 2024, inaelezwa ni pendekezo la kocha mpya wa kikosi hicho, Florent Ibenge, raia wa DR Congo ambaye ameshafanya naye kazi pamoja, wakati huo wakiwa wote katika timu ya Al-Hilal Omdurman kutokea Sudan.

Azam inatafuta beki mwingine wa kushoto kwa ajili ya kusaidiana na, Pascal Gaudence Msindo, ambapo Imoro ni miongoni mwa mabeki bora kwa sasa anayeweza kuleta ushindani, jambo linalowafanya mabosi wa kikosi hicho kuanza kuiwinda saini yake.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza Imoro aliyewahi kuzichezea Bolga All Stars, Karela United na Asante Kotoko zote za kwao Ghana, anamvutia Ibenge kutokana na uchezaji wake hivyo, anamuhitaji tena ili wakafanye kazi wakiwa pamoja.

Hata hivyo, mbali na Imoro ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja uliobakia Singida, ikiwa dili lake litakwama, nyota mwingine pia anayetazamiwa ni aliyekuwa beki wa Yanga, Joyce Lomalisa aliyekuwa anaichezea Sagrada Esperanca ya Angola.

Lomalisa aliyewahi kuchezea pia, AS Vita Club ya kwao DR Congo, Royal Excel Mouscron ya Ubelgiji, GD Interclube Luanda, FC Onze Bravos do Maquis, Wiliete SC na Kabuscorp SC zote za Angola ni mchezaji mzoefu anayeweza kuleta ushindani pia.

Hadi sasa, Ibenge amependekeza majina ya mabeki wa kushoto wawili, Imoro na Lomalisa ambapo mmoja kati yao atajiunga na kikosi hicho, ambacho kinajipanga upya ili kuongeza ushindani katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.