Mhudumu wa baa akutwa amefia nyumba ya kulala wageni

Arusha. Neema Mwakalukwa (33), mkazi wa Muriet jijini Arusha amekutwa amefia ndani ya chumba cha nyumba ya kulala wageni.

Mwili wa Neema aliyekuwa mhudumu wa baa ulikutwa ndani ya chumba hicho jana Julai 24, 2025.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema leo Julai 25, 2025 kuwa jeshi hilo limeanza upelelezi kuhusu tukio hilo.

Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.

Kamanda alipoulizwa iwapo kuna mtu anashikiliwa kuhusika na tukio hilo amesema upelelezi ukikamilika atatoa majibu.

“Masuala ya kama kuna mtu tunamshikilia, subiri taarifa rasmi baada ya uchunguzi tutasema yote yaliyo ndani ya maswali yenu,” amesema.

Elizabeth Samweli, mama mzazi wa Neema alipata taarifa za kufariki dunia kwa mtoto wake baada ya kwenda kwenye nyumba hiyo ya wageni kumtafuta.

“Huyu mtoto (Neema) huwa anabaki kazini usiku na kurudi asubuhi sana nyumbani kulala kwa ajili ya jioni kuja tena kazini. Nashanga leo (jana) hajaja, nikaamua kuja hapa kazini nikapata taarifa za kifo chake,” amesema na kuongeza:

“Nimeumia sana, hasa baada ya kuja hapa kumuulizia wenzake hawanijibu wanachekacheka tu, wakisema amelala, niliamua kumuita kijana wa jirani akaja akapanda juu kwenye upenyo wa mlango ndiyo akagundua kuna mtu ndani ana ameshafariki.”

Amesema: “Nilishangazwa na kitendo hicho nikabaki nimeduwaa, ndipo polisi wakaja wakachukua mwili tukaondoka.”

Amesema mwanaye mwenye watoto watatu alishindwana na mume akaamua kurudi nyumbani ambako aliamua kufanya kazi ya uhudumu wa baa ili kujitafutia mtaji wa kurejea kwenye biashara yake ya awali ya kuuza vitenge mtaani.

George Mwakalukwa, baba mkubwa wa Neema ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kuanzia nyumba hiyo ya kulala wageni.

“Haiwezekani kila mtu hapa aseme hajui kilichompata mwanangu wakati ni mfanyakazi wa hapa na mgeni akija lazima aandikishe, lazima kuna kitu wanajua hawa wenye baa na wahudumu wengine lakini wanaficha,” amedai.