Mufindi. Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa imemhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Shukrani Jafeti (30), mkazi wa Mtaa wa Lumwago baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumjeruhi kwa panga mumewe, Shadrack Mtokoma.
Hukumu imetolewa Julai 23, 2025 na Hakimu Mkazi, Edward Uphoro aliyesikiliza kesi hiyo.
Katika kesi hiyo ambayo nakala ya hukumu Mwananchi imeiona leo Julai 25, 2025, mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na kosa moja la kujeruhi kinyume cha kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 23, 2025, katika mtaa wa Lumwago wilayani Mufindi.
Anadaiwa kwa masukudi alimjeruhi mume wake, Shadrack sehemu ya kisogo kwa kutumia panga.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka siku ya tukio, muathirika na mshtakiwa wakiwa wamelala nyumbani kwao saa 12:00 asubuhi simu ya mshtakiwa iliita na akaikata, ndipo mume wake akaichukua simu, huku akimuuliza ni kwa nini hataki kuipokea.
Mshtakiwa alimuomba mume wake amrudishie simu lakini alikataa, hivyo yakatokea majibizano ndipo mshtakiwa alitoka nje na kurudi na panga akamkata nalo sehemu ya nyuma ya kichwa.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, muathirika alitokwa damu nyingi akazimia.
Ilidaiwa mshtakiwa alidhani amemuua, hivyo alichukua begi na kukimbia lakini muathirika alipata msaada kutoka kwa mtoto wake, Dorcas Mtokoma kwa kushirikiana na majirani ambao aliwaita kumsaidia.
Walimchukua wakampeleka Hospitali ya Mji Mafinga kwa matibabu baada ya kupata fomu namba tatu ya polisi (PF3), kisha akalazwa.
Mshtakiwa alikamatwa Juni 24, 2025 akafikishwa Kituo cha Polisi Mafinga ambako baada ya kuhojiwa alikiri kutenda kosa hilo.
Julai 23, 2025 mshtakiwa alifikishwa mahakamani ambako alisomewa shtaka hilo ambalo alikiri, mahakama ikamtia hatiani kwa kosa hilo linalotokana na wivu wa mapenzi.
“Mahakama hii inamtia hatiani mshtakiwa Shukrani Jafeti, kama alivyoshtakiwa kutokana na kukiri kwake shtaka linalomkabili,” amesema hakimu.
Baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani, kabla ya kusomewa adhabu, Hakimu Uphoro aliuliza upande wa mashtaka iwapo una kumbukumbu zozote za nyuma za uhalifu kumhusu mshtakiwa.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Simon Masinga alisema hawana kumbukumbu zozote za nyuma za makosa ya jinai dhidi ya mshtakiwa.
Hata hivyo, wakili Masinga aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kutokana na kitendo kilichofanyika kwani kingesababisha mauaji.
Alipopewa nafasi ya kuomba shufaa kabla ya kusomewa adhabu, mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana watoto wawili wanaomtegemea.
Pia alidai ni mgonjwa, ana marejesho ya mkopo ambayo anatakiwa kuyarejesha na anamuhudumia baba yake mzazi.
Akitoa adhabu, hakimu Uphoro amesema amezingatia hoja za pande zote mbili, hivyo Mahakama inamhukumu mshtakiwa kifungo cha mwaka mmoja jela ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.