Mstaafu wetu amekuwa akijitahidi mara kadhaa kujiaminisha kuwa yeye ni mzawa na mkazi halisi wa nchi hii aliyoijenga yeye mwenyewe, lakini akiangalia yanayomtokea, anasita na anaishia kujiona ni mkimbizi tu wa nchi hii!
Ukichukulia kuwa ndugu, jamaa, marafiki na Siri-kali yake walishiriki kikamilifu kukifanya kiinua mgongo chake alipostaafu kuwa ‘luku’ ambayo siku mbili tatu tu umeme umeichapa lapa, na hata “Habari gani?” zao kwake sasa zimekuwa bidhaa adimu, asilaumiwe akijiona ni mkimbizi ndani ya nchi aliyoijenga mwenyewe!
Acha ndugu, jamaa na marafiki, lakini yapo mengi ameyafanya kuijenga nchi hii lakini hajafanywa na Siri-kali yake, na yanafikia kumfanya mstaafu aone kwamba hana tofauti yoyote na mkimbizi, tena yule wa kutoka Sudan au Kongo ndani ya nchi aliyojenga mwenyewe na Siri-kali yake kulisahau hili!
Yapo mengi. Tukumbuke kwamba ni Siri-kali hii inayopenda kujinasibu kuwa inaboresha maisha ya mstaafu, huku ikiyaboresha kwa kumfanya aishi kimiujiza kwa kumpa pensheni ya Shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka 21 bila nyongeza yoyote!
Hii laki moja na elfu hamsini ni kutoka mwezi wa pili tu baada ya Siri-kali kujivuuta na hatimaye kuamua kuwa mstaafu wake wa kima cha chini si mkimbizi, na anastahili kupata nyongeza ya Shilingi elfu hamsini kwenye pensheni yake au akubaliane na ushauri uliotolewa na Msiri-kali mmoja wa kuhamia Burundi akiona mambo vipi!
Hilo ni moja. Katika kutaka kuonekana kuwa Siri-kali inawajali wastaafu wake, ikatangaza kuwa itatoa matibabu ya bure kwa wazee wa Taifa wenye umri wa miaka 60 na kuendelea , wastaafu wakiangukia kundi hilo ili kuboresha maisha yao!
Tukafarijika sana, huku tukiamini kuwa itakuwa ni mwisho kwa wazee wa Taifa na wastaafu kuendelea kwenda zahanati kuandikiwa dawa na kisha… kuelekezwa kwa kidole duka la dawa lililo karibu, ili mzee huyu ambaye hela yake ni ya kusaka kwa tochi, akanunue dawa huko ajitibu au awe mkazi wa kudumu wa Kinondoni!
Maneno ya “matibabu ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi” yakaishia kuwa maneno ya kanga na hakuna kilichoendelea, huku wastaafu wengine waheshimiwa kutoka shamba la wanyama wakigharamiwa na Siri-kali kwenda India, Uingereza au Ujerumani kutibiwa mafua yanayomsumbua na pole zake yule mstaafu anayekatwa mguu kwa kisukari chake!
Tukadhani Siri-kali hii inayoweza kuwanunulia viongozi wake magari ya bei mbaya ya Shilingi milioni 500 kwa moja, badala ya ‘dabo kibin’ ya bei rahisi, ingeweza au ilipaswa kujiongeza na kuwanunulia wazee wa taifa bima ya afya, hasa wale wa kule mashambani ambao walilima na kulimaga mazao ya chakula ili kumlisha mstaafu wakati anaijenga nchi! Hawa wanaishia kusikia kusikia tu kuwa kuna keki ya Taifa!
Kulikuwa na hiki kibubu ambacho kilitunza hela zetu tulizokatwa kwenye mishahara yetu wenyewe. Vimeingia hivi vibubu kibao vya dotcom ambavyo fasta vimeingia na kuchukua akiba ya wafanyakazi na kujengea vikwangua anga kibao vinavyotoza kodi inayoeleweka, lakini wastaafu wenye kibao chao hawaelewi chochote!
Mstaafu anakuwa hafaidiki kwa lolote na kodi inayotozwa kwenye magorofa hayo yaliyojengwa kwa akiba yake, ambayo inaelekea sasa ni kwa ajili ya kuwalipa mishahara waajiriwa wa vibubu hivyo na si kupigwa mahesabu ili akiba ya mstaafu iliyotumika kujenga vikwangua anga hivyo imuwezeshe kulipwa japo ya Shilingi laki sita kwa mwezi! Wastaafu wenyewe wamebaki wangapi?
Hazina! Mfuko wa Hazina umekuwa hazina kweli. Wastaafu wanaopokea pensheni kutoka Hazina wameahidiwa pensheni ya Shilingi laki tano kwa mwezi (kama watapewa), huku wastaafu wenzao wakijibamiza na Shilingi laki moja na elfu hamsini yao kwa mwezi!
Kuna mtu anacheza mchezo mchafu wa Gawanya Utawale hapa! Kwa nini mstaafu asijione ni mkimbizi kwenye nchi aliyoijenga mwenyewe?