Dar es Salaam. Ibrahim Kitine ambaye ni Kijana wa Dk Hassy Kitine amesimulia dakika za mwisho za baba yake aliyefariki akiwa usingizini usiku wa kuamkia leo
Kitine aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) amefariki usiku wa kuamkia leo Julai 25, 2025 akiwa nyumbani kwake Osterbay, Mtaa wa Laiboni 24, jijini hapa.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa watoto wake, Ibrahim Kitine amesema baba yao baada ya kumaliza kula jana usiku alikwenda kulala na ndipo alipokutwa na mauti.
“Amefariki wakati amelala, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha yake,” amesema kijana wake huyo kwa huzuni.
Amesema baba yao alikuwa akisumbuliwa na kisukari kwa miaka 40, ingawa kwa miaka mitatu iliyopita alipata Maradhi ya kiutu uzima.
“Jana usiku baada ya kumaliza kula alikwenda kulala, mwenyezi Mungu amemchukua akiwa amelala,” amesema.
Akizungumzia taratibu za mazishi, Ibrahim amesema mwili wa baba yao utazikwa kesho baada ya Sala ya saa 10 jioni kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaa.
“Asubuhi utaletwa nyumbani hapa Osterbay, kutoka Hospitali ya jeshi Lugalo ulikohifadhiwa, kutakuwa na ratiba nyingine hapa, baada ya Sala ya saa 10, baba yetu atazikwa kwenye makaburi ya Kisutu,” amesema.
Akizungumzia maisha ya baba yao baada ya kustaafu, amesema alipenda kukaa na wajukuu na alikuwa mfuatiliaji wa masuala ya kisiasa.
“Alijikita sana kufuatilia masuala ya siasa na nchi yake (Tanzania), katika uhai wake hakuwahi kuacha kufuatilia siasa,” amesema.
Mbali na siasa, Ibra amesema baba yao pia alipenda watoto wake wasome.
“Hakuna kitu kilimfurahisha baba kama masomo, yeye mwenyewe alikuwa msomi, alikuwa na Master’s mbili, ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyingine ya Canada pia ana Shahada ya uzamivu (PhD).
“Katika maisha yake, moja ya vitu vilikuwa vikimfurahisha ni kuona watoto wake tunasoma na kujiongeza,” amesema.
Amesema jambo jingine alilopenda kwa watoto wake ni kuishi vizuri na watu na kuwa na heshima, kuipenda nchi na kuheshimu maoni ya raia wengine.
Amesema baba yao alikuwa akipenda kusema tutafika kila alipozungumza nao.
“Ndilo meno ambalo lazima amalize nalo kuzungumza, hata tukiwa tunakula, katika mazungumzo ya hapa na pale, atahitimisha na neno tutafika akimaanisha hakuna ambacho kitashindika,” amesema.