Mume adaiwa kumuua mkewe kwa kipigo Bukombe

Geita. Mwanamke mmoja, Manila Kiselya (48) Mkazi wa Kitongoji cha Majengo, Kata ya Katente wilayani Bukombe, amefariki dunia baada ya kudaiwa kushambuliwa kwa kipigo na mume wake kutokana na kugoma kumpa fedha alizokopa kwa ajili ya biashara.

Inadaiwa mwanamke huyo alikopa fedha kwenye moja ya taasisi za fedha ili kuongeza mtaji wa biashara yake lakini mumewe alitaka amgawie lakini aligoma kitendo kilichomkasirisha na kuamua kumshambulia kwa kipigo.

Mwenyekiti wa kitongoji hicho Elizabeth Mwenda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo  na kusema limetokea usiku wa Julai 23 nyumbani kwao huko Katente.

“Huyu mama alikopa fedha akitaka kuongeza mtaji sasa alipozipata mume wake akataka ampe lakini huyu mama amezoea kupigwa hii siyo mara ya kwanza  na kila akipigwa akiambiwa atoe taarifa hataki ukimya umesababisha sasa tumempoteza,”amesema.

Amewataka wanawake wanaofanyiwa ukatili kutofumbia macho ukatili na badala yake watoe taarifa mapema kuanzia ngazi ya mtaa ili mhusika aweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Yohana Pius Mkazi wa Majengo amesema baada ya mwanaume huyo kumpiga mkewe alichukua fedha hizo kiasi cha Sh3 milioni nakuondoka na pikipiki yake na kuwaacha watoto ndani.

“Wakati tukio hili linatokea watoto wa marehemu walikua wakiangalia TV na waliona ni kawaida maana wameshazoea mama yao anapigwa na baadaye maisha yanaendelea lakini hii amepigwa na kuondoka kabisa,” amesema.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bukombe, Haruni Kasubi akitoa elimu ya kupinga ukatili kwa wananchi wa kitongoji hicho amewataka kutofumbia macho taarifa za ukatili kwani kukaa kimya kunasababisha uonevu na majanga yanayoweza kuepukika.

“Wakati mama huyu anapigwa majirani walikua wanasikia kelele lakini hakuna aliyeenda kutoa msaada wala kuripoti. Tuendelee kutoa elimu juu ya haki za binadamu lakini watu hawakutoa taarifa, majirani wangepiga hata yowe haya yasingetokea,” amesema.

Kasubi alioongeza kuwa hakuna sababu ya kumdhuru mwenza na kwamba mtu yeyote anayehisi ameshindwa kuendelea na ndoa anaweza kufuata taratibu za kisheria badala ya kutumia nguvu.

Aidha mwili wa mwanamke huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya Bukombe huku Jeshi la Polisi likiendelea kumsaka mwanaume aliyesababisha mauaji hayo.