Mwashinga msimu ujao ni Pamba au Namungo

PAMBA Jiji na Namungo FC zimeingia vitani kuiwinda saini ya kiungo, James Mwashinga ambaye kwa sasa ni mchezaji huru, huku ikielezwa tayari mawasiliano na kambi ya mchezaji huyo yameanza tangu msimu huu ulipoisha.

Nyota huyo aliitumikia Pamba msimu wa 2024-2025 na kukiwezesha kikosi hicho kumaliza nafasi ya 11 na pointi 34 na alisaini mkataba wa mwaka mmoja, jambo linalowafanya mabosi wa Namungo kumhitaji tena baada ya kuichezea pia timu hiyo.

Mwashinga kabla ya kujiunga na Pamba alitokea Namungo aliyojiunga nayo akitokea Biashara United baada ya kuonyesha uwezo mkubwa, ingawa kwa sasa yupo huru, jambo linaloziingiza vitani tena timu hizo mbili.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua kipaumbele cha kwanza cha kiungo huyo ni kuendelea kuichezea Pamba na tayari amepewa mkataba wa mwaka mmoja, huku akiahidiwa pia bonasi zaidi kama sehemu ya ushawishi wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho.

Mmoja wa kiongozi wa Pamba aliliambia Mwanaspoti, hawako tayari kumpoteza mchezaji aliyefanya vizuri msimu wa 2024-2025, hivyo, kwa aliyemaliza mkataba watahakikisha wanamwongezea, ingawa watakaoondoka ni wale walioshindwa kupigania nafasi.

Pamba tayari imeshaachana na nyota kadhaa hadi sasa wakiwemo, Lazaro Mlingwa, Modou Camara, Ibrahim Isihaka, George Mpole, Cherif Ibrahim, Abalkassim Suleiman na Samson Madeleke.